NAIBU
Waziri wa Fedha, Adam Malima, amesema suala la ukusanyaji wa kodi
inayotozwa na Jeshi la Zimamoto linamuumiza kichwa kwa madai kuwa
hawatoi huduma stahiki kwa wananchi wanaowatoza fedha.
Malima alitoa kauli hiyo mjini Bukoba jana alipozungumza na
wafanyabiashara pamoja na wakulima kuhusu mashine za kieletroniki za
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na tozo ya Zimamoto baada ya wananchi
hao kumtaka kuondoa tozo hiyo.
Alisema kodi si tatizo isipokuwa huduma zinazotolewa na jeshi hilo hazifiki kwa wakati na si stahiki.
Awali mmoja wa wafanyabiashara, Julius Mwamba, alihoji katika kikao hicho kuwa wananchi watalipa kodi ngapi.
Mwamba alisema Tanzania kuna majeshi takribani sita wakiliruhusu
jeshi hilo kuendelea kuwatoza kodi baada ya muda majeshi mengine nayo
yatadai kulipwa kodi.
“Sijui suala la Jeshi la Zimamoto kukusanya kodi liliibuka kutoka
wapi, Tanzania kuna majeshi mengi, kila jeshi likianza kudai kodi
tutalipa kodi ngapi?” alihoji mfanyabiashara huyo.
Alisema kodi hiyo haina faida kwa wananchi kwa sababu hawajui matumizi ya fedha hiyo.
Akijibu hoja ya wafanyabiashara hao, Malima alisema jeshi hilo
limekuwa likilalamikiwa mara nyingi na wakulima, viwanda,
wafanyabiashara na wananchi wa kawaida kwa kutotimiza wajibu wake kwa
wakati.
Alisema suala hilo linapaswa kuangaliwa upya huku akisema kuna
tofauti kubwa ya kazi kati ya Jeshi la Zimamoto na polisi ambao wamekuwa
wakifika kwenye migogoro ya wakulima kwa wakati huku mashamba yakiungua
moto zimamoto hawafiki na kuteketea bila msaada licha ya kulipa kodi na
wakati mwingine wakifika huwa hawana maji.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment