Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Byantanzi, wilayani Muleba,
wamemuomba Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka,
kushughulikia mgogoro wa ardhi inayodaiwa kuuzwa kwa mwekezaji.
Wakizungumza na gazeti hili juzi katika kijiji
hicho, wananchi hao walisema uongozi wa wilaya, umewapa muda wa miezi
sita kuhama katika eneo linalodaiwa kumilikiwa na mwekezaji.
Walisema hata hivyo amri hiyo imetolewa bila wao kupewa maeneo mbadala ya kuendesha maisha yao.
Walielezea kushangazwa kwao juu ya taarifa za kuuzwa kwa eneo hilo kwa mwekezaji, wakati uongozi wa kijiji ukiwa hauna taarifa.
Mmoja wa wananchi hao, Faston Benson, alisema
wananchi katika kijiji hicho, wamekumbwa na hofu baada ya kuelezwa kuwa
wanatakiwa kuhama ili kumpisha mwekezaji.
Diwani wao, Khalid Hussein (Chadema) alielezea
kushangazwa kwake juu ya amri iliyotolewa na uongozi wa wilaya hiyo
ikiwataka wananchi, kuhama katika eneo hilo.
Alisema inashangaza kuwa viongozi waliotoa amri hiyo, hawakuwahi kwenda katika kijiji hicho na kuwasikiliza wananachi.
Mwenyekiti wa Kitongozi cha Ntungamo, katika
kijiji hicho, Desdery Hurubano alisema zaidi ya kaya 300 katika eneo
hilo zinaishi kwa hofu kutokana na vitisho vya kuhamishwa.
Aliwasihi uongozi wa wilaya kwenda katika kijiji
hicho ili kusikiliza malalamiko ya wananchi badala ya kuwapa vitisho vya
kutaka wampishe mwekezaji.
Hurubano alisema jambo hilo halikubaliki na kwamba ni vizuri viongozi waka wazi kwa wananchi wa kijiji hicho.
Kiongozi huyo wa kitongoji alisema inashangaza na
kusikitisha kuona wananchi walioishi katika eneo kwa muda mrefu,
waamriwa kuhama bila kushirikishwa.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment