Zana haramu za uvuvi zipatazo 6,347 zenye thamani ya shilingi milioni 781.6 zimekamatwa na kuteketezwa kwa moto katika kipindi cha siku kumi na nne.
Afisa mfawidhi wa kikosi cha doria mkoani Kagera Aporinary Kyojo amesema kuwa zana hizo zilikamatwa katika oparesheni maalum ya kukamata zana haramu katika ziwa Victoria, iliyofanyika kuanzia Februari 3 hadi Februari 16 mwaka huu.
Kyojo ametaja zana haramu zilizokamatwa kuwa ni makokoro 59, nyavu za timba 670, makila 5,570, nyavu za dagaa zenye macho madogo 48 na kamba za makokoro zenye urefu wa mita 51,200.
Amesema kuwa pia katika oparesheni hiyo walikamatwa samaki wachanga aina ya sangara kilogramu 4,648 wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 13.9, mizani mibovu 17, mitumbwi isiyokuwa na usajili mitano na watuhumiwa 13.
Amesema kuwa katika oparesheni hiyo ya pamoja ya kanda ya Afrika Mashariki dhidi ya uvuvi haramu, iliwahusisha maafisa kutoka makao makuu ya wizara ya uvuvi jijini Dar-es-salaam, polisi, wataalam wa uvuvi kutoka mkoani Kagera, kamati za usimamizi wa mialo (BMU) na waangalizi kutoka nchini Uganda.
Oparesheni hiyo ya siku 14 iliandaliwa na mradi wa Smart Fish unaofadhiliwa na jumuiya ya nchi za Ulaya chini ya kamisheni ya bahari ya Hindi (IOC) na kuzishirikisha nchi za Uganda na Tanzania.
0 comments:
Post a Comment