WABUNGE wawili wa Muleba Kusini na Kaskazini, Profesa Anna
Tibaijuka na Charles Mwijage, wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
wameibuka na mbinu mpya ya kupata wananchi kwa kupika na kugawa wali
katika mikutano yao ya hadhara.
Aliyeanza ni Prof. Tibaijuka, ambaye tangu Oktoba mwaka jana alianza
kutembea na sufuria za wali kama njia ya kushawishi wananchi kuhudhuria
mikutano yake na kumsikiliza.
Mwijage ameanza kutumia mbinu hiyo mwaka huu kama njia ya kurejesha
imani ya wananchi kwake na CCM, katika kujaribu kupiku nguvu za Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kinawanyima usingizi
katika majimbo yao.
Kwa mara ya kwanza, Prof. Tibaijuka alizuka na sufuria za wali katika
Kijiji cha Kiga, Kata ya Rulanda, akiwa na magari matatu yenye sufuria
zipatazo sita za wali na kreti kadhaa za soda.
Jana, Mwijage alianza kutumia mbinu hiyo katika Kata ya Kamachumu
ambapo alichinja ng’ombe mmoja na kupika wali kwa wingi kama njia ya
kuvuta wananchi kuhudhuria mkutano kwa wingi.
Tibaijuka na Mwijage wanakabiliwa na upinzani mkubwa majimboni mwao
kutokana na mwamko wa mabadiliko unaosimamiwa na makada na viongozi wa
CHADEMA.
Mikutano yao imekuwa ikikosa mvuto, na watu wanahudhuria kwa uchache,
jambo lililowalazimisha kubuni njia ya kuvuta wananchi kwa kupika na
kugawa wali.
Hata hivyo, mbinu hii imeanza kuwaletea msukosuko katika jamii, kwani
wananchi wanaona kama wabunge wao wanawadharau na kuwahonga chakula.
Wananchi wanataka wabunge hao watekeleze ahadi zao badala ya kugawa
wali, kwani katika ilani ya uchaguzi waliyoinadi mwaka 2010, hakuna
popote walipotangaza kugawa wali kwa wananchi.
Vile vile, baadhi ya wananchi wanadai kwamba kwa hatua hii, Mwijage
na Tibaijuka wameanza kudhihirisha kwamba hawakubaliki kwa kiasi cha
kutumia vivutio vya chakula kuita na kuteka watu.
Mmoja wa wakazi wa Kamachumu waliokerwa na ‘rushwa’ hii mpya, Justin
Kingi, aliliambia gazeti hili jana kuwa: “Mwijage anatafuta watu wapya
awadanganye kwa kutumia wali. Ni mbinu dhaifu ya CCM. Haitafanikiwa.
Hawezi kupata watu wa maana, labda watoto wadogo na wachezaji mpira
ambao watakuwa uwanjani.”
Mkazi mwingine wa Kamachumu, Sylvester Kaboko, alisema: “Amepika kilo
600 za wali na ng’ombe mmoja. Upo wali mwingine umebebwa kutoka Kagera
Sugar, hatujui ni kiasi gani… Hiki ni kituko…. watu wanaendelea na
shughuli zao.”
Habari zinasema aliwapatia waendesha pikipiki sh 1,000 kila mmoja ili
waweke bendera za CCM kwenye pikipiki kupamba maandamano, wengi
wakagoma wakisema hawawezi kujidhalilisha kwa shilingi elfu moja.
Muchunguzi Tibalikwenda, mkazi wa Kijiji Rwanda, akizungumza na
gazeti hili kutoka Kamachumu, alisema: “Wawindaji wanapenda kwenda na
wawindaji wenzao; wachungaji na wachungaji wenzao. Sisi tunataka
maskini mwenzetu, atakayewasilisha maoni yetu kunakohusika. Waendelee na
wali wao, na muziki wao, sisi tuna shughuli zetu za maendeleo.”
Alipotafutwa Mwijage kufafanua tuhuma hizo, aling’aka akidai amefanya
mambo mengi ya maendeleo jimboni na hivyo, asiulizwe vitu vidogo
vidogo kama hivyo
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment