Home » » Wauzaji wa samaki watuhumu kiwanda kwa kuwahujumu

Wauzaji wa samaki watuhumu kiwanda kwa kuwahujumu

Baadhi ya wafanyabiashara wa samaki mjini hapa wamedai mitaji yao inahujumiwa na Kiwanda cha Kuchakata Minofu ya Samaki cha Vicfish, kwa kuwalipa bei ndogo kwa madai kwamba wanapeleka samaki wengi wasio na ubora.
Walalamikaji hao majina yao yanahifadhiwa kwa sababu za biashara, walidai kiwanda hicho kinatumia kisingizio hicho ili kipate sababu ya kununua samaki wao kwa bei ya chini.
Walidai kuwa mbinu hiyo imesababisha wafanyabiashara wengi wa samaki kufilisika.
Waliendelea kuwa samaki wasio na kiwango maarufu reject (wasiofaa) hulazimika kuwauza kwenye kiwanda hicho kwa bei ya Sh250 kwa kilo, badala ya bei ya kawaida ya Sh800 na kwamba, licha ya kupeleka samaki wa viwango sawa, malipo hutolewa kwa viwango tofauti.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, alidai aliwahi kupeleka tani moja ya samaki aina ya sangara na kuambiwa kilo 700 hazikuwa na kiwango cha ubora unaotakiwa na kiwanda hicho, hatua iliyiosababisha kuziuza kwa bei ya Sh250 kwa kilo.
Pia, walidai wanalazimika kuuza kwa bei inayopangwa na mnunuzi kwa sababu baada ya kuwafikisha samaki hao kiwandani, hawawezi kupata soko jingine na mmoja wao kudai mbinu hiyo imemfanya abaki na madeni mengi ya wavuvi.
Hata hivyo, Meneja wa kiwanda hicho, Nurdin Salim alikanusha madai hayo na kwamba, anazo nyaraka zinazoonyesha saini za walalamikaji kwa samaki wasio na ubora wanalipwa Sh800 badala ya 250 kama walivyodai.
Salim alisema baadhi ya wafanyabiashara wanaouza samaki kiwandani hapo hutoa madai yasiyo na ukweli, huku wengine wakidaiwa fedha nyingi na kiwanda na kwamba kama hawaridhiki na bei siyo lazima wauze samaki katika kiwanda hicho.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa