Home » » Maeneo ya Ikulu yageuzwa uwanja wa ngono, ukabaji

Maeneo ya Ikulu yageuzwa uwanja wa ngono, ukabaji

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga.
 
Wananchi wa mtaa wa Pwani katika Manispaa ya Bukoba, wamelalamikia vitendo vya ngono vinavyofanyika katika maeneo ya Ikulu ndogo na kutaka vidhibitiwe kwani  vinaidhalilisha serikali ya mkoa Kagera.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliotishwa na Mwenyekiti wa mtaa huo kuzungumzia hali ya ulinzi na usalama katika mtaa wao, wananchi hao walidai kuna watu wamekuwa wakiegesha magari yao karibu na makazi ya mkuu wa mkoa huo na kufanya vitendo vya ngono ndani ya magari.

Walisema kila siku ikifika saa 12 jioni hadi saa mbili usiku watu wasiofahamika huegesha magari yao na kufanya ngono katika eneo la Gymkhana  na kuliomba Jeshi la Polisi kuwakamata watu hao.

Mbali ya kulalamikia vitendo hivyo vya ufuska katika eneo hilo, pia wamelalamikia wizi wa mara kwa mara unaotokea katika makazi yao ikiwamo vitendo vya kukaba watu, wizi wa mifugo na ukwapuaji kutokana na mtaa huo kuwa karibu na ziwa.

Walisema wezi wamekuwa wakiwapora akina mama fedha wanapokuwa wakienda kununua samaki mwaloni wakati wa alfajiri.

Mwenyekiti  wa mtaa huo, Evord Barnaba alisema kutokana na kukithiri kwa vitendo vya wizi na ngono katika eneo hilo, walilitaarifu Jeshi la Polisi ili kuwakamata wahusika na kuchukua hatua ya kuweka vibao vya kuzuia watu kuegesha magari katika eneo hilo wakati wa usiku lakini vitendo hivyo vinaendelea.

Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uhalifu katika mtaa huo wenye wakazi 1,457 asilimia kubwa wakiwa ni watumishi wa serikali, wananchi hao waliazimia kuchanga Sh.

3,000 kila mmoja kwa kila mwezi kwa ajili ya kuajiri kikundi cha vijana cha kulinda maeneo hayo wakati wa usiku kama njia mojawapo ya kukabiliana na vitendo hivyo. 

Akizungumza katika kikao hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga aliwaagiza mkuu wa polisi wa wilaya na mkuu wa polisi wa tarafa Rwamishenye kuhakikisha zinafanyika doria katika maeno ya Ikulu ndogo ili kudhibiti wizi na vitendo vya ngono katika eneo hilo.

“Sitaki tena kusikia vitendo vya uhalifu vimetokea katika maeneo hayo na ikifika usiku watu wasipite katika maeneo hayo, ni uzembe mkubwa kuruhusu zifanyike ngono na katika maeneo hayo”  alisema kamanda Mayunga.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa