KESI 82 zilizokaa muda mrefu zimefutwa mkoani Kagera kwa kukosa ushahidi wa kutosha katika kipindi cha mwaka 2012/2013.
Akizungumza wakati wa sherehe za Siku ya Sheria nchini, jana
Mwanasheria Mfawidhi wa Serikali Kanda ya Bukoba, Sakina Sinda, alisema
kesi zilizofutwa zilihusisha washitakiwa wa zamani.
Sinda alisema tatizo la kesi hizo kukaa muda mrefu linatokana na
sababu mbalimbali ikiwamo mashahidi kushindwa kufika mahakamani hasa
kesi za jinai.
Alisema ili kuhakikisha tatizo hilo linapungua wanajitahidi
kutembelea magereza yote mkoani Kagera na kupitia majalada, lengo ni
kubaini kesi zilizodumu muda mrefu bila kusikilizwa ili zitolewe
maamuzi.
“Tunajitahidi kukutana na mahabusu, kuwasikiliza na kubaini matatizo
yao, baadaye tunatoa maelekezo ili kesi zao ziharakishwe,” alisema
Sinda.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Gad
Mjemmas, alisema suala la haki kutolewa kwa wakati linakabiliwa na
changamoto ikiwemo sheria za uendeshaji wa mashauri huku akitolea mfano
kifungu namba 225 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Akizungumzia kifungu hicho, Jjaji Mjemmas alisema kinawataka upande
wa mashtaka kukamilisha upelelezi ndani ya siku 60 tangu mshtakiwa
kufikishwa mahakamani lakini hakishughuliki na makosa ya kughushi na
mauaji ya makusudi au ya bila kukusudia.
Alisema hayo husababisha mshitakiwa kukaa mahabusu hata miaka 10 kwa
kisingizio cha upelelezi kutokamilika, ambapo Mahakama hufungwa mikono
kwa kutotoa unafuu kwa mshitakiwa kwa kuwa sheria haijaweka wazi ukomo
wa muda wa upelelezi kwa baadhi ya makosa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment