MKUU wa Mkoa (RC) wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe,
amewataka watendaji wa vijiji na kata kuwafikisha mahakamani wazazi
wanaowaozesha watoto wao chini ya umri na wale wanaowapa ujauzito na
kuwasababishia kutoendelea na masomo.
Kanali mstaafu Massawe alitoa wito huo juzi wakati wa maadhimisho ya
miaka 37 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika kimkoa
wilayani Kyerwa.
Alisema watendaji wa vijiji na kata hawana budi kuwachukulia hatua
watu wanaohusika kuwapa ujauzito wanafunzi na kuwaharibia ndoto zao za
kupata elimu na kuwasababishia umaskini na uduni wa maisha.
“Sitakaa kimya kwa hawa mafataki, nitabanana nao katika kipindi chote
cha madaraka yangu, hata nikitoka madarakani sitawachoka, nitaendelea
kuwalaani kwani ni watu waharibifu kwa watoto wetu,” alisema mkuu huyo
wa mkoa.
Alisema kuna baadhi ya wazazi ambao nao wanachangia kutowapeleka
watoto wao shule kwa visingizio vya ugumu wa maisha, na wengine
kuwaozesha kabla ya umri nao watafikishwa mahakamani watakapobainika
kuhujumu haki za watoto wao.
Alisema serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya shule mbalimbali
za msingi na sekondari kwa ajili ya watoto kupata elimu bora na kwamba
watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kuanza mwaka huu
wataingia darasani bila matatizo, kwa kuwa miundombinu ya kila shule,
vyumba vya madarasa, madawati na walimu vinakidhi kiwango.
Chanzo;tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment