ZAIDI ya wanafunzi 9,000 wilayani Karagwe hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Hali hiyo imebainika kutokana na utafiti uliofanywa na halmashauri ya wilaya hiyo mwaka jana.
Ofisa Elimu Shule za Msingi, Gidion Mwesiga, alibainisha hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Mwesiga alisema utafiti wa kubaini wanafunzi hao ulifanyika Mei
katika shule mbalimbali za wilaya hiyo kwa kushirikisha walimu,
waratibu wa elimu kata na viongozi wa Idara ya Elimu.
Alisema utafiti huo ulibaini wanafunzi 9,786 wasiojua kusoma,
kuandika na kuhesabu ambapo wasichana ni 4,729 na wavulana ni 5,057.
Mwesiga alisema wanafunzi hao ni wa darasa la pili hadi la sita
katika shule 108 za serikali na kata 22 zilizopo wilayani hapa.
Alitaja baadhi ya kata ambazo zina idadi kubwa ya wanafunzi
wasiojua kusoma na kuandika ni Bweranyange (356), Nyakasimbi (386) na
Chanika (453).
Alisema tatizo kubwa la wanafunzi hao kutojua kusoma na kuandika ni
kutokana na utoro, baadhi ya wazazi kutokuwa na mwamko wa elimu na
watoto wengine kutoanzia madarasa ya awali.
Alitaja baadhi ya mikakati iliyoandaliwa na halmashauri hiyo ili
kukabiliana na tatizo hilo kuwa ni kuwakaririsha wanafunzi wote
wasiojua kusoma na kuandika, kutengewa madarasa maalumu na muda maalumu
baada ya saa za masomo kwa ajili ya kufundishwa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment