Home » » CAG amaliza kumkagua meya Bukoba

CAG amaliza kumkagua meya Bukoba



HATIMAYE Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amekamilisha kazi ya siku 35 ya ukaguzi wa tuhuma za ufisadi wa miradi zinazomkabili Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
Akizungumza na Tanzania Daima jana mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, Utouh alisema katika ukaguzi huo wameweza kuwahoji wahusika wote pasipo kuacha mtu.
Utouh alisema kuwa wanatarajia kuweka hadharani ripoti hiyo baada ya wiki tatu kuanzia sasa.
Alisema kuwa wakaguzi watakwenda Bukoba kwa ajili ya kukamilisha hatua za mwisho za ripoti hiyo na baada ya hatua hiyo wataweka hadharani suala hilo.
“Hadi sasa kazi imeshakamilika na tuliwahoji wahusika wote, hivi sasa tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha ripoti, hatutakuwa na siri, kila kitu kitawekwa hadharani,” alisema.
Timu ya wakaguzi hao ilianza kazi Septemba 30, mwaka huu, huku Utouh akiwaonya viongozi wote wanaotuhumiwa kwa namna moja au nyingine pamoja na watendaji wa manispaa hiyo kujiepusha na vitendo vyenye mwelekeo wa rushwa, akisema vinaweza kuvuruga mwenendo mzima wa ukaguzi huo.
Kamati hiyo ilifanya kazi kwa kuegemea hadidu 14 za rejea huku wakijikita katika maeneo husika kwa mwaka wa fedha 2010/11 hadi 2012/13.
Kwa mujibu wa Utouh, hadidu hizo ni kuchunguza usahihi wa utaratibu uliotumika kumpata mwekezaji wa kituo cha kuoshea magari, yaani Kampuni ya ACE Chemicals Ltd, kuchunguza uhalali wa nyaraka na kiasi kilichowekezwa cha sh milioni 297 kwenye mradi huo.
Nyingine ni kuchunguza tatizo na sababu zilizosababisha viwanja 800 kutogawiwa kwa wananchi waliochangia gharama za upimaji, mradi wa upimaji wa viwanja 5,000, mradi wa ujenzi wa soko na mradi wa kujenga kitegauchumi.
Aliongeza kuwa nyingine ni mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi, ujenzi wa chuo cha ualimu, kituo cha maarifa na ujenzi wa bwawa kwa ajili ya utalii.
Yalikuwepo pia masuala mengine ya matumizi ya fedha yanayoashiria ubadhirifu na wizi au ufujaji wa mali za halmashauri na kutoa ushauri kwa serikali kuhusu namna bora ya kuimarisha usimamizi wa mapato katika halmashauri hiyo.
Ukaguzi huo pia umegusa mradi wa maji wa Benki ya Dunia kwa ajili ya Kata ya Nyanga, kiwanja cha Shule ya Msingi Kiteyagwa, barabara ya kupitia Kagondo Kaifu hadi Kagondo Karagulu, ujenzi wa Soko Kuu la Manispaa ya Bukoba na Ilani ya Uchaguzi.
Chimbuko la mgogoro huo ni madiwani kumlalamikia meya wao kuwa ameiingiza manispaa katika ufisadi kwenye miradi kadhaa.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani.
Vilevile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka.
Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi wa kiasi cha sh milioni 134 za ujenzi wa kituo cha mabasi.

Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa