Home » » Uongozi Kasharunga lawamani

Uongozi Kasharunga lawamani



WANAVIJIJI wa vijiji viwili wa kata ya Kasharunga, wilayani Muleba, mkoani Kagera, wameulalamikia uongozi wa vijiji hivyo kwa madai ya kuuza ardhi ya kijiji kinyume cha sheria huku wakishindwa kuwashirikisha wanakijiji hao kuhusu fedha za ruzuku za vijiji hivyo. Wakizungumza katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na diwani wa kata hiyo, Khalid Hussein, wananchi hao walidai kuwa hawana imani na viongozi wao kwa kuwa wamekuwa wakiuza ardhi kwa watu wa mikoa mingine pasipo kuwashirikisha wanakijiji.
Wanakijiji hao walidai kuwa viongozi  hao wameshindwa kutoa taarifa za mapato na matumizi ambapo ardhi inayodaiwa kuuzwa ilitengwa kwa ajili ya kujenga wodi ya wagonjwa.
Akizungumzia suala hilo mtendaji wa kijiji cha Nkomero, Pastory Sulusi, alidai kuwa amekuwa akiandika muhtasari wa vikao mbalimbali vikiwemo vya uuzaji wa ardhi lakini umekuwa ukibadilishwa.
“Unakuta mkutano wa kijiji umeuza ardhi hekari tano lakini mwenyekiti amekuwa akibadilisha muhtasari na kuandika ya kwake huku akiwauzia hekari zaidi ya 150 bila kuishirikisha serikali ya kijiji na mkutano mkuu hata mtendaji mwenyewe,” alidai.
Akijibu tuhuma hizo kwa niaba ya Mwenyekiti Edward Kimanzi wa kijiji cha Nkomero, Angelo Mselika, ambaye alikaimu nafasi hiyo alisema tuhuma hizo amezisikia wamekuwa wakimshauri kiongozi huyo kuitisha mkutano lakini jambo hilo limeshindwa kutekelezwa.

Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa