Home » » DC Misenyi adaiwa kuhujumu Hifadhi ya Taifa Minziro

DC Misenyi adaiwa kuhujumu Hifadhi ya Taifa Minziro

Chapa
Mkuu wa Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Kanali Mstaafu Issa Njiku
Mkuu wa Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Kanali Mstaafu Issa Njiku na afisa maliasili Jamesi Matekere wanadaiwa kuhujumu Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Asili wa Minziro kwa kuruhusu tani zaidi ya 200,000 kuvunwa kwa kutoa vibali kwa wafanyabiashara isivyo halali.

Vijiji vilivyonufaika na vibali hivyo kwa kisingizio cha kujenga makanisa, vituo vya polisi, mahakama, matanki ya maji ni pamoja na kijiji cha Minziro, Nyakahanga, Kalagala, Kigazi, Kiwelu ambapo kila mfanyabiashara alitakiwa kutoa Sh. 200,000 za kutuma maombi bila kutolewa risiti.

Akiongea na NIPASHE, Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Minziro, Mkama  Waswa, alisema ana kibali na. KGR/C.4/26/120 cha  22/01/2013 na kuwa walipofika wanajeshi, polisi na jamaa wa usalama wa taifa katika operesheni tokomeza ujangili walidai kibali hicho ni feki na kuwa endapo watampeleka mahakamani ataomba mkuu huyo wa wilaya aunganishwe katika kesi yake na afisa maliasili.

Akiongea na NIPASHE kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, msemaji wa wizara hiyo, Rumisha Chikamdi alisema ni makosa kutoa vibali katika hifadhi ya Minziro na kuwa wanaangalia uwezekano wa kuzuia vibali hivyo.

Kwa mujibu wa kibali cha serikali cha 22/01/2013 kumb. na. KGR/C.4/120 na kibali na. KGR/C.4/26/121 cha  25/01/2013, wakuu hao wameruhusu kupasuliwa mbao ndani ya hifadhi hiyo aina ya afrocarpus dawei (Podo), mimusups bagshawei na beilshrmedia ganaensis.

Wakiongea na NIPASHE kwa nyakati tofauti mkuu huyo wa wilaya, Njiku na Matekere wamekiri kutoa vibali vya uvunaji ndani ya msitu huo kwa maelezo kuwa sheria za misitu zinawalinda kwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo ni Mwenyekiti wa kamati ya uvunaji. 

Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya viongozi wa serikali wilayani Misenyi kutoka Idara mbalimbali za serikali wakiwamo polisi na maliasili ndiyo wenye vijana wa kupasua mbao katika hifadhi hiyo ambapo huwalinda kuhakikisha wako salama muda wote.

Mbao za msitu huo huuzwa Bukoba na nchini Uganda ambapo maafisa maliasili huzigonga nyundo kuonyesha kuwa serikali imepokea kodi jambo ambalo siyo sahihi.

Kama alivyoeleza Mtendaji wa serikali ya kijiji cha Misenyi, Eliud Tibaijuka na Mwenyekiti wake, Bonifasi Lugemo, licha ya kuwa na vibali vingi katika kijiji chao hawajawahi kulipa ushuru wa kijiji, halmashauri na serikali kuu kama sheria za misitu zilivyoelekeza ili kibali kiweze kuwa halali.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa