WANANCHI wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bukoba
vijijini mkoani Kagera wamekumbwa na taharuki kubwa baada ya askari
mgambo kujifanya maofisa wa Operesheni Kimbunga awamu ya tatu, huku
wakijitambulisha kama maofisa Usalama wa Taifa na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA).
Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti
hili, mgambo hao walifika katika maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Rubale wakiwa
wamevalia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Akizungumza na Tanzania Daima, Shaban Buruan ambaye
ni mmiliki wa duka la bidhaa mbalimbali, alisema akiwa dukani kwake lilifika
kundi la watu, wengine wakiwa wamevalia sare za JWT na wengine
kiraia, wakamueleza kuwa ni maofisa wa Operesheni Kimbunga awamu ya
tatu, wakiongozana na mtendaji wa Kijiji cha Kihumulo, Gidius Alfred.
Buruan alisema baada ya kujitambulisha, walimuomba
leseni ya biashara huku wale waliokuwa wamevalia kiraia wakijitambulisha kama
maofisa wa TRA.
Alisema kuwa hakuwapa leseni hiyo kwa vile hakuwa
nayo mahala hapo, na hivyo wakamtaka awape fedha sh laki moja, jambo ambalo
hakuliafiki badala yake akaomba muda awaletee, lakini waliondoka.
Naye Clementina Kakooza ambaye ni raia wa Rwanda
aliyeolewa Tanzania, alisema mgambo hao walifika kwake wakiwa na sare za JWTZ
wakiongozana na mtendaji wa kijiji na kumtaka awaonyeshe vibali vyake vya
kuishi nchini la sivyo watamfikisha polisi.
“Waliponitishia hivyo niliwaeleza
kuwa nimebaki kutokana na agizo la serikali kuwa watu tulioolewa na
Watanzania tubaki wakati tukifanya utaratibu wa kupata vibali, walikataa na
kusema kuwa niwapatie kiasi cha sh 500,000 ambacho sikuwa nacho.
“Nikataka niwape ng’ombe wawili na mbuzi mmoja
wakagoma na kulazimisha niwapatie fedha, hapo ndipo tuliposhituka na kupiga
simu polisi Rubale,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip
Kalangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Oktoba 26 mwaka huu, katika Kijiji
cha Kihumulo, Tarafa ya Rubale, Halmashauri ya Bukoba.
Alisema kuwa baada ya Operesheni Kimbunga awamu ya
pili kitaifa kumalizika, walikabidhi majukumu yote kwa kamati ya ulinzi na usalama
za vitongoji, kata, wilaya na mkoa kuendelea na taratibu za kubaini wahalifu wa
makosa mbalimbali.
Kalangi alisema wakiwa katika maeneo mbalimbali ya
kutekeleza majukumu ya kikazi, walipata taarifa kuwa kuna mgambo walionekana
wakifanya kazi ya kukamata watu na kuwahoji, hususani wahamiaji haramu.
Walifika eneo la tukio na kufanikiwa kuwakamata mgambo watatu.
Aliwataja waliowakamatwa kuwa ni Amran Sadick,
Abeid Amada na Mathias Sospeter ambao ni mgambo wa Manispaa ya Bukoba na Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Kihumulo, Gidius Alfred.
Alisema mtendaji huyo alikamatwa kwa kosa la
kushirikiana na mgambo hao kufanya kazi bila kushirikiana na uongozi wa kata na
wilaya.
Kwa mujibu wa Kalangi, walipofikishwa polisi na
kuhojiwa hawakuwa na la kujitetea zaidi ya kuomba msamaha.
Alisema watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani kwa
kosa la kudai fedha kwa njia ya vitisho na uchunguzi unaendelea ili
kuendelea kubaini makosa yao mengine kwa ajili ya kuwasilisha ushahidi
mahakamani.
Hata hivyo, alifafanua kuwa wakati watuhumiwa hao
wanakamatwa, hawakuwa na sare za jeshi lolote na kwamba uchunguzi bado
unaendelea.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment