Home »
» Wahamiaji warudi kwa kasi Kagera
Wahamiaji warudi kwa kasi Kagera
Katika
hali isiyo ya kawaida, wahamiaji haramu waliorejeshwa nchini mwao na
serikali katika ‘Operesheni Kimbunga’ wameanza kurejea kwa wingi katika
Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera wakijiita M23 na kupora mali za wananchi
kwa nguvu.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Benedict Kitenga, aliyasema
hayo jana wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa huo Kanali mstaafu,
Fabian Massawe ambaye alitembelea wilaya hiyo kukagua shughuli za
maendeleo na ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za kata.
Alisema
wahamiaji hao wamejazana katika Kijiji na Kata ya Kibingo wakiwatisha
wananchi ambao hivi sasa wanahofia usalama wa maisha yao na mali zao.
Aliongeza
kuwa, baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kupata taarifa
hizo, ilikwenda eneo la tukio na kufanya operesheni kubwa na kufanikiwa
kukamata wahamiaji haramu zaidi ya 20 na baadhi ya Watanzaia waliokuwa
wakiwahifadhi.
Mhandisi Kitenga alisema baada ya kukamatwa,
wahamiaji hao walirudishwa katika nchi zao bila kutaja uraia wao na
Watanzania waliohusika kuwahifadhi wamechukuliwa hatua za kisheria.
“Kutokana na hali ilivyo, wananchi wanapaswa kutoa taarifa wawaonapo wahamiaji haramu katika maeneo yao,” alisema.
Kwa
upande wake, Bw. Massawe alisema, katika “Operesheni Kimbunga”,
wahamiaji haramu walirudishwa katika nchi zao, lakini operesheni hiyo
inaendelea ili kuhakikisha waliobaki wanakamatwa na kurudishwa nchini
mwao.
“Chini ya Kaulimbiu ya Hakuna wa Kubaki na Hakuna wa Kurudi,
tutahakikisha kila mhamiaji haramu anaondoka na Watanzania ambao
watabainika kushirikiana nao pia watachukuliwa hatua za kisheria.
“Naiagiza
Kamati za Ulinzi na Usalama kuendelea na operesheni hadi wahamiaji
haramu wamalizike,” alisisitiza Bw. Massawe na kuwataka wananchi watoe
taarifa kwa viongozi wanapowaona na kutoa namba zake za simu.
Hata
hivyo, baadhi ya wananchi waliohojiwa walisema tatizo la wahamiaji
haramu linachangiwa na baadhi ya watendaji wa Serikali ngazi za chini
ambao wanachukua hongo na kuwarudisha.
Walisema inavyoonekana,
viongozi wa chini kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji hadi kata, wamepewa
mamlaka makubwa pia wamekuwa wakikaa muda mrefu bila kubadilishwa vituo
vya kazi na hivyo kujenga mazoea na wahamiaji hao.
“Serikali
kuanzia ngazi ya Wilaya, iwe na utamaduni wa kuwatembelea viongozi wa
vitongoji na kata kwa kushtukiza ili kukomesha tabia hii ambayo
wamejijengea na kuonekana miungu watu katika maeneo yetu,” alisema mkazi
wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Hivi
karibuni Serikali ilifanya “Operesheni Kimbunga” na kushirikisha vyombo
mbalimbali vya ulinzi na usalama baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa wiki
mbili kwa wahamiaji haramu wawe wameondoka nchini kwa hiari yao.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment