Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania,(IGP) Said Mwema
Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Henry Mwaibambe, alimtaja aliyeuawa kuwa ni Hassan Mhongoli (38) na kuwa mauaji hayo yalitokea Jumamosi iliyopita saa 3:45 usiku katika eneo la hoteli ya Bukoba Coop inayomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera (KCU 1990 Ltd).
Mwaibambe alisema kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kumetokana na taarifa kutoka kwa raia wema ambapo walianza kumfuatilia na kufanikiwa kumkamata juzi saa 9:00 mchana akiwa amejificha nyumbani kwake eneo la Uzunguni katika Manispaa ya Bukoba.
Alisema baada ya kumkamata alionyesha bastola aina ya Glock yenye namba PCH589 anayoimiliki kihalali ambayo inadaiwa aliitumia katika mauaji hayo na kudai kuwa alifikia uamuzi huo baada ya kupigwa ngumi na marehemu.
Alisema kuwa kampuni ya Sigara siku hiyo walikuwa na sherehe ya familia ambayo ilimalizika saa moja jioni na kwamba baadhi ya wafanyakazi waliondoka katika eneo hilo na kumwacha Hassan akiwa na mfanyakazi mwenzake, Amon Lyimo (40).
Alisema watu hao walikaa katika hoteli hiyo hadi saa 3:45 ndipo waliingia katika gari la kampuni, lakini walipoanza kuondoka ghafla ilitokea teksi na kuziba njia. Alisema walipiga honi, lakini haikuwapisha.
Alisema kutokana na kitendo hicho wafanyakazi hao wa Sigara walishuka katika gari na kuanza kuzozana na waliokuwa katika gari hilo na kwamba baadaye alishuka mtu mmoja na kuanza kupigana nao na baadaye kutoa bastola na kumpiga risasi Hassan kichwani na kufariki dunia papo hapo.
Alisema katika purukushani hizo mfanyakazi mwingine wa Sigara, Amon Lyimo, alitaka kuwamua, lakini naye alipigwa risasi mkono wa kulia na ametibiwa katika Hospitali ya Mkoa na kuruhusiwa jana.
Mwaibambe alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi na kuwa bastola hiyo ilikutwa na risasi tano na waliokota maganda mawili ya risasi eneo la tukio.
Mwili wa marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera ukisubiri kuchukuliwa na ndugu na jamaa kwa ajili ya mazishi.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment