Home » » Waziri Magufuli atajwa kesi ya wizi wa pembejeo

Waziri Magufuli atajwa kesi ya wizi wa pembejeo

Waziri wa Ujenzi, Dk,John Magufuli
 
Kesi ya ubadhilifu wa fedha za pembejeo za kilimo inayowakabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Chato, Hadija Nyembo, aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hamida Kwikwega na wenzao watatu, imechukua sura mpya baada ya mawakili wa washitakiwa kumtaja Waziri wa Ujenzi, Dk, John Magufuli, kuhusika.
Hatua hiyo imefuatia Mahakama hiyo kuanza kupokea ushahidi wa upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kelvin Murusuri.

Shahidi namba moja ambaye ni mchunguzi wa Takukuru, Said Bakari (39), alidai kuwa kwa kipindi cha mwaka 2010/11 washitakiwa hao walitenda makosa mbalimbali ikiwemo kutumia madaraka yao vibaya kisha kumteua wakala wa usambazaji wa pembejeo asiye na sifa.

Alisema mshitakiwa namba moja Nyembo ambaye alikuwa mkuu wa wilaya ya Chato kabla ya kuhamishiwa Uvinza, akiwa Mwenyekiti wa kamati ya pembejeo ya wilaya hiyo alihusika kuwapitisha wazabuni wa usambazaji wa pembeo wasio na sifa katika kikao kilichofanyika Julai 6, mwaka 2010.

Alidai kuwa mshitakiwa namba mbili Kwikwega anayetetewa na wakali wa kujitegemea Deogratias Rutahindurwa, alidaiwa mahakamani kupitisha baadhi ya nyaraka za kuwatambulisha mawakala waliopitishwa kinyume cha sheria na kamati ya pembejeo ya wilaya kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.

Wengine waliofikishwa mahakamani ni aliyekuwa Ofisa Kilimo na Mifugo wa wilaya hiyo, Dk. Pheres Tongora, ambaye pia aanashitakiwa kuteua na kuwapitisha mawakala wasio na sifa.

Wengine ni mshitakiwa namba nne aliyekuwa wakala wa usambazaji wa pembejeo kata ya Buseresere, Mery David pamoja  na Kaimu mtendaji wa kijiji cha Mapinduzi, Mageni Mbassa.

Shahidi huyo aliwasilisha vielelezi vinne zikiwemo barua na mihutasari ya vikao vya kamati ya pembeo vilivyoketi na kupitisha maamuzi ya kuwapata mawalala wa usambazaji bila kufuata taratibu za manunuzi ya umma.

Baada ya mashahidi wa kwanza kumaliza kuwasilisha ushahidi wake, wakili wa Rutahindurwa alitaka kujua sababu za Waziri wa ujenzi na mbunge wa jimbo la Chato,Dk Magufuli kushindwa kuhusishwa katika mashitaka hayo licha ya kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya pembejeo ya wilaya hiyo.

Alisema iwapo kamati ya pembejeo ilifanya maamuzi yasiyo fuata taratibu kanuni na sheria za manunuzi iweje baadhi ya wajumbe wake akiwemo Dk. Magufuli wasihusishwe kwenye mashitaka hayo.

Wakili anayemtetea Mery David,Tuguta Fadhili alihoji kuwa kama kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kutokana na shinikizo la Waziri wa Ujenzi Dk. Magufuli.

Alidai kuwa iwapo kikao cha kamati ya pembejeo kiliyoketi Julai 6, 2010 kilikuwa halali iweje maamuzi yake yaonekane hayakuwa sahihi na kumhusisha pia mshitakiwa namba mbili (Kikwega) ambaye siku ya kikao hicho hakuwapo katika maamuzi hayo.

Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Jovith Katto baada ya upande wa washitakiwa kumaliza kuhoji maswali yao mahakama hiyo iliahilishwa kwa ajili ya kupokea ushahidi wa mashahidi namba mbili ambaye ni Ofisa Ugavi wa wilaya hiyo, Machage Mwema.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa