Home » » Ulaji wetu na maradhi ya kisukari-3

Ulaji wetu na maradhi ya kisukari-3

Tulijifunza katika makala mbili zilizopita kuwa binadamu hawezi kuishi bila ya kula vyakula vyenye wanga, mafuta na protini.
 Njia za kuyakabili maradhi ya kisukari
Tunaweza kuyakabili maradhi ya kisukari kwa njia kuu nne. Mosi, kuwa na elimu kuhusu maradhi ya kisukari na mtu kuwa na uwezo wa kujipima kiwango cha sukari mwilini mwake.
Pili, ni kula mlo kamili, tatu kufanya mazoezi na nne ni kupata tiba sahihi ya maradhi ya kisukari.
Njia hizi ni muhimu kuzifahamu kwa wagonjwa wa kisukari na wale ambao hawajapatwa na maradhi hayo, yanayoongezeka kwa kasi duniani kutokana na maisha ya kisasa kama vile kula vyakula vyenye mafuta, sukari na chumvi nyingi.
Kama umepatwa na kisukari
Ingawa maradhi ya kisukari yana kishindo kikubwa, lakini watu waliopatwa na ugonjwa huo wanashauriwa wasichanganyikiwe wala kuhuzunika. Kufanya hivyo ni kuongeza maradhi katika miili yao.
Wanachotakiwa ni kuukabili ugonjwa huo kwa kujiamini. Na hilo litawezekana endapo wagonjwa hao wataelekeza nguvu zao katika kuujua ugonjwa huo kwa undani.
Kujua huko kutawafanya wabadili mtindo wa maisha yao kama vile kula mlo kamili, kufanya mazowezi, kuacha kunywa pombe, kunywa maji ya kutosha, kulala muda wa kutosha, kudhibiti hasira na msongo wa mawazo.
Wapi utapa elimu?
Elimu kuhusu maradhi ya kisukari inaweza kupatikana kwa njia mbalimbali kama vile kusoma vitabu na magazeti, kusoma katika mitandao ya kijamii, kuhudhuria semina, kusikiliza vipindi vya mada hiyo kutoka katika redio na luninga.
Vilevile, elimu ya ugonjwa wa kisukari inaweza kupatikana kwa wataalamu wa maradhi hayo waliopo katika kniniki za kisukari na hospitali mbalimbali.
Baadhi ya wagonjwa wa kisukari pia, wanaelimu kubwa ya maradhi hayo baada ya kuhangaika kwa muda mrefu kuitafuta elimu hiyo na uzoefu wao wa maisha kama wagonjwa.
Kuujua ugonjwa wa kisukari
Kama tunavyofahamu, binadamu ameweza kuleta mapinduzi makubwa katika maisha yake tangu enzi za zana za mawe mpaka sasa, enzi za dijitali kutokana na elimu.
Ni dhahiri pia, kuwa tutaweza kuyakabili maradhi ya kisukari kikamilifu kama tutakuwa na uwelewa wa kutosha juu ya maradhi hayo.
Tufahamu nini kama wananchi?
Kujua tunakokukusudia hapa sio kama vile wanavyofahamu wataalamu wa afya.
Wananchi wajue maana ya ugonjwa wa kisukari, aina za kisukari, sababu za kupata maradhi ya kisukari na dalili za kisukari.
Halikadhalika, watu wanatakiwa watambue hali gani mtu akiwa nayo (risk factors) yuko katika hatari ya kupata maradhi ya kisukari kama vile unene uliopitiliza, kuwa na shinikizo la damu, kuwa na msongo wa mawazo, ujauzito, kutokufanya mazoezi au kazi za kutoka jasho, na kuwa na miaka arobaini au zaidi.
Zaidi ya hayo, watu wanatakiwa wazijue athari mbaya za ugonjwa wa kisukari kama vile kuharibika kwa viungo vingine mfano macho, viungo vya uzazi, figo, mishipa ya fahamu na moyo.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa