Home » » `Sheria ya kuzuia shughuli za siasa vyuoni itazamwe upya`

`Sheria ya kuzuia shughuli za siasa vyuoni itazamwe upya`

Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoani Kagera,Pius Ngeze.
 
Serikali imeshauriwa kuiangalia upya Sheria ya Vyuo namba 7 ya mwaka 2005 inayozuia kufanya mikutano na shughuli za vyama vya siasa ndani ya maeneo ya vyuo.
Ushauri huo ulitolewa na mwakilishi wa wanachuo wa Chuo Kikuu cha St. Augustine (Saut) tawi la Sokoine Kampasi ya Bukoba, wakati wa hafla ya kukabidhi kadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wanachuo 42 wa chuo hicho waliojiunga na chama hicho.

Risala ya wanachuo hicho ilisomwa na mwakilishi wao, Silas Malima, mbele ya mgeni rasmi, Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoani Kagera, Pius Ngeze.

Malima alisema wanakabiliana na changamoto ya Sheria Vyuo Vikuu Namba 7 ya mwaka 2005.

Kwa mujibu wa Malima, sheria hiyo inayozuia kufanya mikutano na shughuli za vyama vya siasa ndani ya maeneo ya chuo.

Kwa msingi huo, Malima aliishauri serikali kuitazama upya sheria hiyo kwa lengo la kuirekebisha.

Kwa upande wake, mgeni rasmi Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoani Kagera, Ngeze, mbali ya kukabidhi kadi hizo kwa wanachama wapya 42 wa chuoni hapo, pia aliwataka wanachama hao wapya  pamoja na wa zamani, kuhakikisha kwamba wanawaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi.

Ngeze alisema vile vile, viongozi wa Chama wanapaswa kuwaeleza wananchi ukweli huo kwani  vinginevyo viongozi wa upinzani watawaeleza  na kupindisha mafanikio hayo au kuyafanya ni yao.

Ngeze aliyataja baadhi ya mafanikio hayo yalifanywa na serikali chini ya CCM kuwa ni pamoja na usambazaji wa umeme vijijini na mijini, usambazaji wa maji safi na salama mijini na vijijini, mawasiliano ya simu, ujenzi wa barabara za lami na changarawe vijijini na mijini.

Mengine ni usafiri na usafirishaji wa barabara, reli na anga, upanuzi na uboreshaji wa elimu ya msingi, sekondari, vyuo na vyuo vikuu.

Aidha, Ngeze alisema jukumu la tawi la CCM katika vyuo vikuu hususani tawi la Saut Bukoba, ni pamoja  na kujenga na kukiimarisha Chama ndani ya Jumuiya ya Chuo Kikuu; kuongeza idadi ya wanachama na kufanya vikao kwa mujibu wa katiba.

Pia aliwataka viongozi na wanachama waendelee kujiendeleza ili kuwaongoza watu; wasome magazeti wasikilize redio, waangalie televisheni na washiriki majadiliano mbalimbali.

 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa