Halmashauri ya wilaya ya Missenyi mkoani Kagera
imetoa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 60.1 kwa vikundi mbalimbali vya
wanawake na vijana katika kipindi cha miaka sita iliyopita.
Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa halmashauri
hiyo Elzaberth Kitundu imesema kuwa mikopo hiyo imetolewa kuanzia mwaka wa
fedha 2007/2008 hadi 2012/2013.
Kitundu amesema kuwa katika kipindi hicho vikundi
vya akina mama vilipatiwa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 40.8 ambapo
vikundi vya vijana vilipatiwa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 19.3.
Amesema kuwa lengo la halmashauri hiyo kuviwezesha
vikundi vya wanawake na vijana kwa kuwapatia mikopo ni kutaka
kuinua mitaji yao, na kuwa hali ya marejesho kwa vijana sio mbaya
isipokuwa kwa upande wa wanawake ndio wanarejesha kwa kusuasua.
Amesema kuwa katika kuhakikisha vikundi hivyo
vinakuwa endelevu, wamekuwa wakiwashauri wanachama wake kuanzisha vyama vya
akiba na mikopo (SACCOS) na kuwa katika wilaya hiyo hadi sasa kuna vyama vya
ushirika 73, vikiwamo vya mazao 28, Saccos 36 ambapo vyama tisa ni vya
mchanganyiko.
0 comments:
Post a Comment