Home »
» Wanasiasa wamchefua January Makamba
Wanasiasa wamchefua January Makamba
Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw.January Makamba,
amekemea tabia ya baadhi ya wanasiasa nchini kutumia mkondo wa dini
kisiasa kwani hilo ni kosa
kubwa kwa mustakabali wa amani ya nchi.
Bw. Makamba aliyasema
hayo juzi Mjini Bokoba, mkoani Kagera, wakati akizungumza kwenye Tamasha
la Amani ambalo liliandaliwa na Nazareth Singers kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali.
Alisema wanasiasa wenye
tabia hiyo wanaamini kuwa waumini wa dini yake watamuunga mkono katika
uchaguzi jambo ambalo ni hatari kwa sababu anapogombea uongozi, wananchi
ndio wanaopiga kura bila kujali dini zao.
Aliongeza kuwa,
viongozi wa dini wamefanya kazi kubwa ya kulinusuru Taifa kutokana na
chokochoko za kidini kupitia mahubiri yao kwani bila wao, hali ingekuwa
mbaya zaidi.
Aliwaomba viongozi wa
madhehebu ya dini nchini, kuendelea kuhubiri amani, upendo na mshikamano
miongoni mwa Watanzania ili kudumisha amani iliyoasisiwa na Hayati
Julius Nyerere.
"Baada ya kuibuka kwa
chochoko za kidini nchini, viongozi wa dini wamefanya kazi kubwa ya
kuhubiri amani, upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi...mahubiri
yao
yamesaidia kupunguza chokochoko hizo," alisema.
Bw. Makamba alisema madhara ya Taifa kukosa amani ni makubwa na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuheshimu imani za watu wengine.
Alikemea tatizo la
ukosefu wa haki na usawa katika jamii juu ya upatikanaji wa huduma
mbalimbali za msingi ikiwemo elimu na afya miongoni mwa Watanzania.
"Unapoona katika jamii
hakuna haki na usawa hilo ni tatizo,kwa mfano, ukiona kuna watu wanapata
elimu au huduma tofauti na wanayopata wengine, uhakika wa amani
unakuwa hatarini," alisema.
Aliwapongeza waandaaji
wa tamasha hilo ambalo liliwakutanisha waumini wa dini mbalimbali mkoani
humo na kusisitiza kuwa, ujumbe uliotolewa usambazwe nchi nzima.
Aliahidi kusaidiana na waandaaji hao kuhakikisha ujumbe huo wa amani unafika maeneo mbalimbali nchini.
Awali Mkuu wa Mkoa huo,
Kanali mstaafu Fabian Massawe,alisema amani ya Tanzania ipo mashakani
kutokana sababu mbalimbali kama malumbano ya kidini, kisiasa, matumizi
ya dawa za kulevya kwa unyanyasaji wa kijinsia.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment