MKUU wa Wilaya ya Muleba, Lembris Kipuyo, amewaagiza maofisa ugani
wa halmashauri hiyo kuwa na mavazi ya shambani yaliyowekewa nembo ili
watambulike kwa wakulima.
Kipuyo alitoa agizo hilo katika kongamano la mtandao wa vikundi vya
wakulima wadogowadogo (Mviwata) mkoani Kagera la kuibua changamoto za
kilimo lililofanyika wilayani hapa.
Mkuu huyo wa wilaya (DC), alisema lengo la kutaka kuwepo na vazi
maalum la kuwatambua maofisa ugani linatokana na maafisa ugani walio
vijijini kufanana na wakulima, hivyo kuwapa wakati mgumu baadhi ya
wakulima kuwatambua pindi wanapowahitaji.
Alisema wataalam hao wa kilimo ni wachache katika halmashauri hiyo
yenye vijiji 161 ambao hawatoshelezi mahitaji ya wakulima kwa wakati
kutokana na ukosefu wa miundombinu ya usafiri.
Alisema wilaya hiyo iko kwenye mkakati wa kuwawezesha maofisa ugani
wachache ambapo mmoja ataweza kuhudumia vijiji vitatu na kuwafikia
wakulima kwa ukaribu zaidi kwa kuwapatia pikipiki.
Alisema mpango huo utasaidia ukusanyaji wa takwimu za kilimo kupitia
maafisa ugani kwa kuwezeshwa usafiri na vitendea kazi vya kutosha.
Mbali na hilo, aliwatahadharisha wakulima kuhusu kuhifadhi mazingira
na kuwataka kuacha tabia ya kulima kwenye vyanzo vya maji.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment