na Antidius Kalunde, Bukoba
VIJANA mkoani Kagera wameshauriwa kujishugulisha na kazi mbalimbali za kuwaletea maendeleo na kutakiwa kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ili kuwasaidia kutatua matatizo ambayo yanawakabili kimaisha na kukabiliana na tatizo kubwa la ajira kwa vijana.
Mwenyekiti wa shirika la Maejor Alliance Education Center (MAEC) la mkoani Kagera linalojishugulisha na kupambana na dawa za kulevya hasa kwa vijana, Godfrey Innocent, alitoa ushauri huo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo ikiwemo utawala bora wa asasi na usimamizi wa fedha kwa wanachama wa shirika hilo.
Alisema kuwa kwa hivi sasa nguvu kazi nyingi ya vijana imepotea kutokana na kujihusisha na madawa ya kulevya ikiwemo uvutaji wa bangi unywaji wa pombe uliokithiri jambo ambalo limesababisha vijana kukumbwa na wimbi la umaskini.
Innocent aliongeza kuwa shirika hili la MAEC linajitahidi kwa kasi kubwa kuhakikisha linawashawishi vijana kutambua athari za utumiaji wa madawa ya kulevya na kuwataka wapinge utumiaji huo na kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Edwin Sebastian alisema jumla ya wanachama 45 wamenufaika na kupata mafunzo ambayo yamefadhiliwa na shirika la the Foundation for Civil Society ambao wao ndio watakuwa mabalozi wazuri kwa vijana wengine mkoani Kagera na kuongeza kuwa mbali na kutoa elimu watapata uongozi bora usimamizi wa fedha na uandishi bora wa miradi.
Aliongeza kuwa shirika hilo lililoanzishwa mwaka 2007 mkoani Kagera limewanufaisha jumla ya vijana 1250 kwa kuwapa elimu bora na kuwanusuru na utumiaji wa dawa za kulevya na wao kuendelea kuwashauri vijana wengine.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment