Home » » USAFIRI KUTOKA KAGERA KWENDA KIGOMA WAREJEA

USAFIRI KUTOKA KAGERA KWENDA KIGOMA WAREJEA

Na Renatha Kipaka, Bukoba
WAKAZI wa Kagera wanaotegemea huduma ya usafiri kati ya Miji ya Bukoba na Kigoma wamepewa uhakika wa kuwapo na huduma hiyo, baada ya kumalizika kwa mgogoro baina ya Kampuni za Bukoba Express na Vislam, uliodumu kwa mwezi mmoja.

Akizungumza mjini hapa jana, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) mkoani Kagera, Japhet ole Simaye, alisema huduma hiyo imerejeshwa na itakuwa ya uhakika kwa kila wiki.

Alisema tatizo la upatikanaji wa huduma ya usafiri wa kila siku kati ya Mji wa Bukoba na Kigoma lilisababisha abiria wa sehemu hizo kukosa huduma ya usafiri.

Alisema mgogoro uliokuwapo kati ya watoa huduma hiyo ni wa kupinga kuingiliwa katika ratiba zake za kusafirisha abiria ambazo ni Jumatatu, Jumatano na Ijumaa ambao ulipingwa na Kampuni ya Bukoba Express.

Kutokana na mgogoro huo, ushauri uliopata muafaka ni kuishauri Kampuni ya Bukoba Express kusafirisha abiria Jumanne, Alhamisi na Jumamosi, utaratibu uliotolewa hapo awali na kampuni hiyo kuupinga.

Julai, mwaka huu, SUMATRA walichukua hatua kwa kuwanyang’anya leseni ya usafirishaji wa abiria na kuwarudishia Agosti, baada ya kuomba msamaha na kukubali masharti ya kulipa faini ya Sh 250,000.

Aidha, amewataka wasafiri mkoani Kagera kuondoa shaka juu ya huduma za usafiri, kwa kuwa ofisi hiyo iko tayari kusimamia sheria.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa