Home » » MAZISHI YA RUGAMBWA KUGHARIMU MIL. 200/-

MAZISHI YA RUGAMBWA KUGHARIMU MIL. 200/-



na Mwandishi wetu
MAZISHI ya kihistoria ya masalia ya mwili wa Kardinali wa kwanza barani Afrika, Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa, yatagharimu sh milioni 200.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema masalia ya mwili wa Kardinali Rugambwa yatahamishwa kutoka Kanisa Katoliki la Kashozi yalikohifadhiwa kwa miaka 15 iliyopita na kuzikwa rasmi katika Kanisa Kuu la Bukoba, ambalo ukarabati wake umekamilika.
Alisema kiasi hicho cha fedha kitatumika katika shughuli za mazishi pamoja na uzinduzi wa mfuko wa elimu wa Kardinali Rugambwa.
Alisema shughuli ya kuhamisha masalia ya mwili wake uliozikwa Desemba 17 mwaka 1997 itafanyika Oktoba 6, mwaka huu na kufuatiwa na maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwake, Oktoba 7, mwaka huu.
“Lengo ni kupata sh milioni 200 ambazo zingine zitakuwa kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa elimu wa Rugambwa. Fedha hizi tunaziomba kutoka kwa Watanzania wote watakaopenda kuchangia na tayari tuna kamati jijini Dar es Salaam na Kagera zinazopokea na kuratibu michango na safari ya kuja Bukoba kwa shughuli hiyo,” alisema Askofu Kilaini.
Alisema mfuko huo wa elimu utaanzishwa kwa lengo la kumuenzi, kwani enzi za uhai wake, Kardinali Rugambwa alihamasisha elimu na kujenga shule mbalimbali ikiwemo Shule ya Sekondari ya Rugambwa, ujenzi wa seminari kuu ya Ntungamo, Segerea na shule nyingine nyingi nchini ambazo hadi leo zinafanya vizuri.
Askofu Kilaini alisema wanatarajia kupata wageni wengi wa ndani na nje ya nchi ambapo Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, marais wastaafu, mawaziri, mabalozi wa nchi mbalimbali ndani na nje ya nchi, wafanyabiashara na watu mashuhuri ni miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kushuhudia tukio hilo.
Kardinali Rugambwa alizaliwa mwaka 1912 katika Kijiji cha Rutabwa na kupata upadri mwaka 1948. Alipata ukardinali mwaka 1960 na kufariki dunia Desemba 8 mwaka 1997 na kuzikwa Kashozi Desemba 17 mwaka 1997.
Kabla ya kifo chake, Kardinali Rugambwa aliagiza mwili wake uzikwe katika Kanisa Kuu la mjini Bukoba, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likijengwa upya kwa ajili ya kuuzika mwili wake.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa