Home » » MAUAJI YA DIWANI MULEMA YACHOCHEA VURUGU

MAUAJI YA DIWANI MULEMA YACHOCHEA VURUGU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Kimwani, Muleba mkoani Kagera, wamevamia, kuharibu mali na kuchoma moto nyumba nane katika tukio linalohusishwa na ulipaji kisasi na chuki za kisiasa.
 
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya kutokea mauaji ya diwani wa kata hiyo. Sylvester Muliga (55) kupitia CUF.
 
Mwenyekiti wa kijiji Kyota lilipotokea tukio hilo, Daud Kiluma, alisema wananchi hao walivamia nyumbani kwa aliyekuwa mgombea udiwani wa CCM, Alex Rwakayonza, wakimtuhumu kuhusika na mauaji hayo na kuharibu mashine ya kusaga nafaka pamoja na mashine nyingine ya jirani.
 
Kiluma alisema wananchi hao walivamia nyumba hiyo na kuanza kubomoa milango na kuingia ndani kisha kuchoma moto mali zilizokuwamo na hatimaye kufyeka migomba na kuvunja vioo vya gari lake.
 
Alisema baada ya hapo, wananchi hao walikwenda kwa washirika wa karibu wa Rwakayonza, akiwamo mtoto wake, na kuchoma moto nyumba nane za watu hao.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba jeshi la polisi limeimarisha ulinzi katika eneo hilo.
 
Aidha, Kamanda Ollomi alisema katika tukio la mauaji ya diwani huyo, hadi jana watu watatu walikuwa wamekamatwa, baada ya mmoja kukamatwa jana. Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni Adelard Anthony (42) na Shilanga Gunzari (22)
Diwani Muliga alivamiwa nyumbani kwake usiku wa kuamkia juzi na  kukatwa katwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda Ollomi alisema diwani huyo, wakati akiangalia taarifa ya habari saa mbili usiku nyumbani kwake, watu wasiofahamika waliingia wakiwa na silaha mbalimbali za jadi na kuanza kumshambulia.
 
Majirani walipopata taarifa za kuvamiwa kwa diwani huyo, walifika nyumbani kwake kwa lengo la kumpatia msaada lakini walikuta tayari amejeruhiwa vibaya, hivyo kumuwahisha katika hospitali ya Kagondo  kwa ajili ya matibabu. 
 
Kutokana na majeraha makubwa aliyokuwa ameyapata, ilipofika saa saba usiku, alifariki dunia wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa