Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WALENGWA wa Mpango wa Uhawilishaji wa fedha za ruzuku kwa kaya
masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) III wa
kunusuru kaya masikini wilayani Kyerwa, wamelalamikia ucheleweshwaji wa
fedha kutoka benki wakati wa malipo ambao umeonekana kuwa kero na
kuwakatisha tamaa wahusika hao.
Walitoa malalamiko hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella
aliyefanya ziara ya siku moja kwa lengo la kupata maelezo juu ya
maendeleo ya mpango na mafanikio yaliyofikiwa na kutafuta ufumbuzi juu
ya changamoto zinazokabili mpango huo ili malengo ya Serikali ya
kupunguza umasikini yafikiwe kwa asilimia 100.
Mkazi wa kijiji cha Mulongo, Adelina Danstan alisema mwanzoni wakati
wanaingizwa katika mpango huo walielezwa kuwa dirisha la malipo
linafunguliwa na kufungwa ndani ya siku nne, lakini kwa Wilaya ya Kyerwa
ni tofauti ambapo hufunguliwa siku nne lakini malipo hufanyika siku
mbili au moja usiku na mchana.
“Wenzetu wakianza kupata malipo sisi hushinda vituoni siku mbili jua
kali au mvua ikiwa halali yetu tukisubiri malipo ambapo tunalazimika
kuwauliza wahusika wa Tasaf ambao tunaelezwa kuwa benki ndiyo
inayokwamisha na kusababisha hali hiyo hata wao hawapendi hali hiyo
itokee,” alieleza Dastan.
Mkazi wa kijiji cha Rwabikagati, Catherine Binomutonzi alisema
kutokana na adha hiyo inayoelezwa kuwa inasababishwa na benki kutotoa
kipaumbele kwa wilaya hiyo husababisha walengwa kuhudhuria vituoni siku
mbili na kutoka patupu; na siku ya tatu jioni ndipo fedha zinapoletwa na
kuanza kugawiwa mpaka usiku.
“Hali hii inakatisha tamaa na kuona kama tunadharauliwa kwa kuwa ni
masikini, kwa hiyo tunakuomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati na kuona ni
sababu zipi zinakwamisha. Kumbuka ucheleweshwaji huo unasababisha
msongamano, wazee hapa wanashindwa kubaki mpaka usiku wakihofia maisha
yao kuwa hatarini kwani wanaweza kukabwa na vibaka usiku kwa hiyo
wanalazimika kuondoka na kuiacha fedha,” alisema Binomutonzi.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment