Home » » 8 WASIMAMISHWA KAZI BUKOBA.

8 WASIMAMISHWA KAZI BUKOBA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Bukoba, limewasimamisha watumishi wanane kutokana na ufisadi wa Sh milioni 851 zilizotolewa na Serikali pamoja na wafadhili kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella ameagiza kuchukuliwa hatua za kijinai kwa watendaji wote waliohusika. Mongella alishtushwa na taarifa ya tume iliyoundwa na uongozi wa mkoa huo kuchunguza matumizi ya fedha hizo kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo limekaa kikao cha dharura na kuwasimamisha watumishi hao ili kupisha uchunguzi. Waliosimamishwa ni aliyekuwa Mganga Mkuu (DMO), Hamza Mgula kabla ya kuhamishiwa Manispaa ya Bukoba, Idara ya Fedha ni Mweka Hazina, Jonathan Katunzi na Selialisi Mtalemwa, Kitengo cha Ujenzi; Robert Massoro na Deus Bizibu, Ofisa Mipango na Ofisa Elimu Sekondari, Lucas Mzungu, Idara ya Mipango, Mustapha Sabuni na Idara ya Mifugo, Dk Kisanga Makigo.
Hali hiyo ilikuja wakati Mwenyekiti wa Tume ya watu sita, Wambura Sabora kutoa taarifa katika kikao maalumu cha madiwani, watumishi wa halmashauri hiyo, wakuu wa idara kutoka mkoani na mkuu huyo wa mkoa juu ya waliyobaini ndani ya siku nne walizofanya ukaguzi na uchunguzi ambapo walidai kubaini madudu.
“Katika uchunguzi tulibaini kuwa fedha kutoka Basket Fund milioni 307 zilizotolewa na Serikali 2011/2012 kwa ajili ya kununulia dawa katika hospitali na vituo vya afya zilihamishwa na kutumika tofauti na malengo bila kufuata taratibu zinazostahili huku milioni 200 za Mfuko wa Barabara zilizotolewa 2014 kwa ombi maalumu ambazo zilizotolea kwa mfumo wa kibajeti hazikutumika kama ilivyokusudiwa na badala yake zilihamishiwa sehemu nyingine ikiwemo matumzi ya ofisi,” Wambura alisema.
Alitaja fedha nyingine kuwa ni Sh milioni 168 za Mfuko wa Jimbo ambazo pia zimetumika katika shughuli nyingine, bila idhini ya kikao chochote wala nyaraka inayoonesha kuhamishwa kwa fedha hiyo jambo ambalo ni kosa kisheria kwani ni matumizi yanayotia shaka.
Baada ya Mkuu wa Mkoa kupata taarifa hiyo, aliwataka Mweka Hazina, John Katunzi kutoa maelezo, na akakiri kuwepo kwa upungufu huo huku akibainisha walibadilisha matumizi ya fedha hiyo baada ya kukaa na Mkurugenzi wakati huo Glades Ndyamvunye.
Inaelezwa kuwa walipanga kurudisha fedha hizo lakini hadi sasa hazijarudishwa. Pamoja na hayo, alimwagiza Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) Mkoa, Joseph Mwaiswelo na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo kuwachukulia hatua zaidi watuhumiwa kwa yale yatakayobainika kuwa ya kijinai.
CHANZO ; HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa