Home » » KAGASHEKI:PINDA NI DHAIFU

KAGASHEKI:PINDA NI DHAIFU

Asema kwa miaka miwili ameshindwa kuchukua hatua
  Shabibi naye apigilia msumari, akataa kuunga mkono bajeti
Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM),Balozi Khamis Kagasheki,
 
Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Balozi Khamis Kagasheki, amemtupia lawama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa kushindwa kutumia nafasi yake kutatua mgogoro wa Manispaa ya Bukoba na kukaa kimya huku akiendelea kumtambua Meya Anatory Amani, ambaye alijiuzulu kisha kukana maamuzi yake.
Amani alijiuzulu wadhifa wake miezi mitano iliyopita baada ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi katika manispaa hiyo na kugundua matumizi mabaya ya fedha za halmashauri hiyo.

Balozi Kagasheki alitoa lawama hizo jana wakati akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2014/15 na kusema kuwa mgogoro huo unaitia aibu serikali kwa kuwa Amani alijiuzulu Januari, mwaka huu mbele ya viongozi wa mkoa wa Kagera, lakini baadaye alitangaza kuwa kurejea madarakani kinyemela.

Hata hivyo, alimshukuru Rais Jakaya Kikwete na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuingilia katika kuchukua hatua katika mgogoro huo kwa kuagiza mamlaka husika kuchukua hatua, lakini ofisi ya Waziri Mkuu ilishindwa kuchukua hatua zozote na kwamba haikuwatendea haki wananchi wa manispaa hiyo.

Alisema CAG alitoa ripoti yake na kutokana na ripoti hiyo, Amani alitamka mbele ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), CAG, Mkuu wa mkoa wa Kagera  na viongozi wengine kisha alitangaza kuwa alijiuzulu, lakini baada ya muda alikana maamuzi yake na kudai kuwa bado ni meya.

”Hakuishia hapo, aliitisha kikao na waandishi wa habari na kusema hajajiuzulu na hakuishia hapo, alimtukana, akamtukana CAG na serikali na hivi sasa ninapozungumza anaendelea na uongozi...inasikitisha kwa serikali yetu katika kusimamia na uendeshaji wa mambo, hakuna kilichofanyika wala kauli ya serikali kuwa alishajiuzulu,” alisema Balozi Kagasheki.

Alisema Aprili 30, mwaka huu, Katibu Tawala wa mkoa wa Kagera alimwandikia Katibu Mkuu Tamisemi, akieleza kuwa ofisi ya Mkuu wa mkoa inaelewa kuwa meya huyo alijiuzulu katika nafasi yake na kueleza kuhusu yanayoendelea ili kama kuna maamuzi yoyote yatolewe.

Balozi Kagasheki alisema maamuzi yamefanyika, lakini utekelezaji umekuwa tabu na kwamba wakati wa kuhitimisha Bajeti hiyo, Pinda atoe maelezo kama serikali inamtambua kama Amani ni meya au la kwa kuwa mgogoro huo hauna manufaa yoyote.

Balozi Kagasheki alisema Manispaa ya Bukoba  haina bajeti bali imepachikwa kwenye bajeti ya Mkuu wa Mkoa kwa miaka miwili sasa na hakuna vikao vya madiwani vilivyofanyika na kusema kwamba hiyo ni aibu.

Balozi Kagasheki alisema kuwa inashangaza mgogoro huo kutofanyiwa kazi licha ya maamuzi na mapendekezo ya CAG kufanyika, lakini hatua zinashindikana kuchukuliwa na Waziri Mkuu.

”Wananchi wa Manispaa ya Bukoba wamekuwa ni watoto wapweke ambao ofisiya Waziri Mkuu haikuwajali sana, mgogoro umekuwapo tangu Aprili mwaka 2012 …mwaka 2014 ni zaidi ya miaka miwili,” alisema na kuongeza:

“Mgogoro umekuwapo bila kuwa na suluhisho, bila uwezo wa kulitatua...bado mnataka watu wa Bukoba wafurahie kuwa mnawajali, Rais anazungumzia maamuzi yakifanywa yasikilizwe, leo huwezi kuwaambia serikali inawajali wakati hakuna kinachofanyika."

”Mimi mwenyewe nilikuwa waziri kwenye serikali, haya yakanikuta sasa mbunge wa kawaida itakuwa namna gani...suala hili lipo kwenye Kamati Kuu ya CCM kwa muda mrefu,” alisema.

Mara baada ya Balozi Kagasheki kuzungumza, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Paulina Gekul, alisema kuwa suala hilo lililetwa kwenye Kamati ya LAAC ikapitishwa kinyemela baada ya kujadiliwa juu juu, lakini wakati Mbunge wa Jimbo hilo anazungumza Waziri Mkuu alikuwa anapiga 'story' na kwamba tatizo kama hilo lipo Halmashauri ya Ilemela na kuomba mwongozo kama Pinda anaruhusiwa kuendelea kuongea wakati mambo ya msingi yanazungumziwa.

Naibu Spika, Job Ndugai, alikemea baadhi ya wabunge wanaokwenda kuzungumza naWaziri Mkuu wakati masuala muhimu anayopaswa kuyasikia yanazungumzwa na kwamba ataanza kuwakataza wabunge wanaozungumza na Waziri Mkuu na kumfanya asisikilize vizuri.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema Waziri Mkuu ndani ya Bunge hilo ni Mbunge, Kiongozi wa Shughuli za serikali Bungeni na kwamba shughuli za serikali zinaendelea na ndani ya Bunge hilo kuna pande mbili za walioko serikalini na wasiokuwapo.

”Kuna consultation (mashauriano) muhimu sana, lazima ziendelee, haiwezekani kiongozi wa shughuli za serikali kwenye jengo hili na siyo nje, kwa vyovyote nakubalina na ushauri wenu kwa wenye maoni ya kauwaida ya kiofisi wanaweza kusubiri na kwenda ofisini kwake,” alisema Lukuvi.

SHABIBY, KESSI WAMVAA PINDA
Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, alisema hataunga mkono bajeti ya Waziri Mkuu kwa kuwa kwenye jimbo lake serikali imekuwa ikitoa ahadi hewa za kukabiliana na tatizo la maji.

”Kila mwaka kwenye Bajeti ya Waziri Mkuu najibiwa serikali imefikia asilimia 80 hadi 84, wananchi wangu wananunua maji galoni la lita 20 kwa Shilingi 1,000, kila Waziri ni ahadi na mipango mingi isiyotekelezeka,” alisema.

Shabiby alisema Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, alifika kwenye jimbo hilo akiwa ameambatana na wataalamu mbalimbali, lakini hadi sasa hakuna maji na kwamba hataunga mkono bajeti ya wizara yoyote ambayo haitekelezeki.

Alisema Waziri Mkuu ndiye hajafika kwenye jimbo hilo kutoa ahadi na kwamba baadhi ya viongozi wa CCM wanamshutumu kuwa amekula fedha hizo.

Mbunge wa Nkasi (CCM), Alli Kessy, alisema Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, aliwadanganya wananchi wa vijiji vya Namanyere na Machi kuwa watapata majisafi na salama.

Alisema serikali inafanya sherehe kubwa kwa gharama kubwa na kuacha kupeleka huduma muhimu kwa wananchi na wao kuishi peponi na wananchi kuishi mbunguni na kwamba bajeti ya Waziri Mkuu kwa kiasi kikubwa ielekezwe kwenye majimbo yaliyoaachwa nyuma kimaendeleo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa