JAMII imetakiwa kufanya mabadiliko chanya katika elimu kwa kuwekeza
na kupeleka watoto shule ili kuongeza uhamasishaji wa ufaulu mzuri kwa
wahitimu ambao utasaidia kuchangia maendeleo ya haraka.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na mmiliki wa Shule ya Awali
na Msingi ya New Vision iliyoko Kata ya Mugajwale, Tarafa ya Rubare,
Wilaya ya Bukoba, Prosper Nduke, alipozungumza na Tanzania Daima.
Nduke alisema kumekuwa na mwamko hafifu katika jamii kuhusiana na
suala la elimu, badala yake wazazi na jamii nyingi zimekuwa zikitumia
muda na rasilimali kubwa kwa ajili ya mambo yasiyokuwa na tija.
Alisema wengine wamekuwa wakisifia na kuzitamani shule zinazotoa
elimu bora, lakini wakiwa hawajali, wala kulipa ada na michango
inayotakiwa.
“Ili taifa letu lipige hatua, hasa katika ulimwengu wa sasa wa
teknolojia, lazima tubadilike kwa kufuatilia maendeleo yao na
kuwajibika kwa kila jambo maana elimu ni gharama,” alisema Nduke.
Alieleza kuwa aliamua kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuanzisha
shule hiyo mwaka 2003 ili kuinua elimu kwa watu waishio vijijini, hasa
kwa wasichana waliokuwa wanafanya kazi za ndani.
Hata hivyo, Nduke ametoa rai kwa baadhi ya wamiliki wa shule kuacha
tabia ya kuwakaririsha mitihani watoto ili kuwajengea uelewa zaidi na
kuwezesha taifa kupata wasomi na wataalamu wenye uwezo wa kusaidia
kuleta maendeleo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment