ZAIDI ya wavuvi 30 wa Kisiwa cha Mazinga, Kata ya Mazinga wilayani
Muleba, wameandamana hadi kituo cha polisi cha wilaya, kulalamikia
kutokuwepo ulinzi katika Ziwa Victoria, kiasi cha kutoa mwanya kwa
majambazi kuwavamia na kuwapora zana za uvuvi.
Wakizungumza na Tanzania Daima mbele ya kituo cha polisi, wavuvi hao
walisema wameamua kuandamana kutokana na kuongezeka kwa uvamizi huo,
huku Jeshi la Polisi likionekana kutochukua hatua madhubuti za
kuimarisha ulinzi.
Walisema mwishoni mwa wiki iliyopita kundi la majambazi liliwavamia
wavuvi watano na kuwashambulia kwa mapanga, kisha kuwapora zana zao za
uvuvi zenye thamani zaidi ya sh milioni 60.
Katika shambulizi hilo, majambazi hao waliwajeruhi Nicolaus Cleophas
(33), Amidu Hussein (32 ), Mussa Antony (28) Medson Muhanika (30) na
Juma Said (40 ) wote wakazi wa Mulumo Mazinga.
Walidai pia kuwa hivi karibuni kundi la majambazi wenye silaha za
moto lilivamia kisiwa hicho na kupora zana za uvuvi mbalimbali,
zikiwemo injini za mitumbwi sita zenye thamani ya sh milioni 18 pamoja
na kuwajeruhi kwa mapanga wavuvi sita.
Imedaiwa kwa majambazi hao wamekuwa wakifanya uporaji kila
wanapojisikia kwa kuwa wanajua Jeshi la Polisi wilayani humo haliwezi
kufanya chochote.
Thomas Josia, mmoja wa wamiliki wa mitumbwi, alisema wakati wa kutoza
kodi mbalimbali serikali inakuwa ya kwanza kufika visiwani humo huku
wavuvi wakiwa mstari wa mbele kulipa, lakini serikali inakwama kuchukua
hatua za haraka kuwalinda.
Diwani wa Kata hiyo, Alex Bakenjela, alisema wamezungumza na Jeshi
la Polisi ambapo wamekubaliana kushirikiana ili kubaini chanzo cha
ujambazi huo na njia za kukabiliana nao.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, George Mayunga, alisema hana taarifa
za kuvamiwa kwa wavuvi hao, lakini akaahidi kulifuatilia suala hilo
ili walipatie ufumbuzi kwa lengo la wananchi wafanye kazi zao bila
hofu.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment