CHAMA cha Wananchi (CUF) Wilaya Bukoba Mjini, mkoani Kagera,
kimewataka wanachama na wakereketwa wa chama hicho kuhamasishana kukipa
nguvu chama pamoja na kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi
katika uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu.
Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa la
CUF, Saverina Mwijage, alipokuwa akitoa salamu kwa wajumbe wa mkutano
mkuu wa wilaya uliofanyika katika Manispaa ya Bukoba.
Mwijage ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, aliwataka
wananchi wilayani Bukoba kutokata tamaa na badala yake wakitetee chama
mbele ya Watanzania.
“Kwa kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa unakaribia, nawaomba wapenzi,
wakereketwa na wananchi wote kwa ujumla kuanza kujiandaa kwa kuwabaini
wanachama ambao wanaweza kujitokeza kuwania nafasi za uongozi, kwani
msingi wa chama cha siasa kuwa na nguvu ni kuanzia kuchukua madaraka
katika serikali za mitaa,” alisema.
Alisema kwa kipindi ambacho amekuwa nje ya Bunge, kuna mambo mengi
amejifunza yanayohusu maendeleo ya wananchi wa Bukoba na
yanayomshawishi kuanza kuhamasisha wananchi wa Bukoba kupigania chama,
ili kiweze kuwainua kiuchumi wananchi.
“Bukoba imegubikwa na migogoro kila siku, wananchi hawapati kile
kilichotarajiwa. Migogoro haimsaidii mwananchi, mimi nimeazimia
kusaidiana na chama changu kutatua kero hizo,” alisisitiza Mwijage.
Katibu wa CUF Wilaya ya Bukoba Mjini, Ramadhan Bahati, aliwataka
vijana, wanawake na wapenzi wa CUF wilayani humo kuanza kurudisha nguvu
ya chama hicho kuanzia ngazi za kata.
Alisema dhamira ya chama hicho ni kurudisha nguvu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment