WAVUVI wa Kisiwani Mazinga, Kata ya Mazinga wilayani Muleba,
Kagera, wamelilamikia Jeshi la Polisi kwa kutoweka ulinzi wa kutosha
katika Ziwa Victoria hali inayosababisha wavuvi hao kufanyiwa vitendo
vya uhalifu na kuuawa.
Walisema hayo jana walipozungumza na waandishi wa habari baada
ya kuona jeshi hilo halichukui hatua kuhusu taarifa za kunyang’anywa
zana zao za uvuvi, zikiwemo injini za boti katika tukio la hivi
karibuni.
Mvuvi Misana Ramadhani mkazi wa mwalo wa Kimoyomoyo, Kijiji cha
Mazinga, alisema hivi sasa wamechoshwa na vitendo vya uhalifu
wanavyofanyiwa kila mara.
Thomas Josia ambaye ni mmiiki wa mitumbwi, alisema serikali wakati wa
kutoza kodi mbalimbali inakuwa ya kwanza kufika visiwani na wavuvi
wanakuwa mstari wa mbele kulipa kodi, lakini suala la usalama wao
haijali.
“Rais Kikwete wakati wa ahadi zake alisema atapambana na uhalifu
katika sekta ya uvuvi, lakini tunashangaa hakuna kinachoendelea hadi
sasa badala yake tunazidi kuporwa mali zetu… tutaishije wakati ulinzi
unapelekwa nchi nyingine wazawa tunateseka?” alihoji Josiah.
Diwani wa Mazinga, Alex Bakenjela, alisema baada ya Jeshi la Polisi
kuona kilio cha wavuvi hao, limekubali na kushauri kuwepo kwa polisi
jamii watakaobaini chanzo cha tatizo.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, George Mayunga, alisema hajapata
taarifa hiyo kutoka wilayani, huku akiahidi kufuatilia suala hilo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment