Home » » RC MASSAWE AKEMEA WANAOBAGUA WAZEE

RC MASSAWE AKEMEA WANAOBAGUA WAZEE

 
MKUU wa Mkoa (RC) wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe amewataka wahudumu wa afya kuacha tabia ya kuwabagua wagonjwa wenye kadi za bima ya afya, hususani wazee wakati wanapofika vituoni kupata huduma.
Massawe alitoa onyo hilo wakati wa uzinduzi wa mkutano wa Siku ya Wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), uliofanyika mjini Bukoba juzi.
Alisema kuwa yapo malalamiko ya wagonjwa ambao ni wanachama wenye kadi za NHIF kwamba wanabaguliwa wanapokwenda kupata matibabu kwenye hospitali na vituo vya afya vilivyotengwa kwa ajili hiyo, wakitakiwa kutoa fedha taslimu.
“Ubaguzi wa aina yoyote hasa pale mtu anapohitaji kupata huduma ya msingi ambayo ni haki yake hautakiwi, sisi kama watoa huduma tunaposhindwa kutoa huduma kwa wananchi kikamilifu ni kuwakatisha tamaa wanaochangia huduma, mfano mfuko huu,” alisema.
Massawe alisema kuwa wazee hao wanachama wa mfuko huo wanakatwa kiasi kikubwa cha fedha katika mishahara yao kwa ajili ya kugharimia matibabu kwa hiyo wapate huduma bora kama walivyo watu wengine.
Aliliomba Bunge kuweka kifungu kwenye katiba mpya ili kila mwananchi ajiunge na Mfuko wa Bima ya Afya kwa ajili ya kupata matibabu bora ya gharama nafuu.
 Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa