RAIS John Magufuli ametoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vya mafuta
nchini, kuhakikisha kwamba wanafunga mashine za kielektroniki za kutolea
risiti (EFDs) na kuonya watakaoshindwa kufanya hivyo watahatarisha
biashara zao.
Ametoa agizo hilo jana alipohutubia mkutano wa hadhara mjini
Biharamulo mkoani Kagera wakati wa kuzindua barabara ya Kagoma –
Biharamulo – Lusahunga yenye urefu wa kilometa 154, ambayo itasaidia
kuifungua Tanzania na nchi za jirani katika ukanda huo wa Magharibi.
Katika maagizo yake, pia amewataka wakuu wa mikoa na wilaya
kulisimamia jambo hilo kwa karibu. “Kwa muda mrefu baadhi ya
wafanyabiashara wanaoendesha vituo vya mafuta, wamekuwa wakikwepa kodi.
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha kwamba Watanzania
wanapata huduma muhimu ikiwemo afya na elimu,” alisema Rais Magufuli.
Aliongeza, “Hatuwezi kufanikiwa katika hayo kama baadhi ya
wafanyabiashara wanakwepa kulipa kodi na kuacha mzigo mkubwa kwa
watumishi wa umma na wakulima kwa miaka yote.”
Dk Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kuhakikisha vituo vyote vya mafuta
nchini vinatumia mashine hizo. Alisisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka
agizo hilo, vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tangu wiki iliyopita, imeendesha
kampeni ya kufungia vituo vya mafuta visivyotumia EFDs baada ya kuwapo
makubaliano na wafanyabiashara hao tangu Oktoba mwaka jana kufunga
mashine hizo.
Juzi, TRA ilieleza kuwa vituo 710 vya mafuta vilifungwa nchi nzima
tangu ianze kazi ya kuvikagua vituo hivyo kuona kama vinatumia EFDS.
Aidha, vituo 469 kati ya hivyo vimefunguliwa baada ya kukidhi vigezo
vilivyowekwa na TRA na vituo vingine 241 havijafunguliwa kutokana na
kushindwa kukidhi masharti ya TRA.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, serikali imeongeza bajeti ya kununulia
dawa muhimu kutoka Sh bilioni 31 hadi Sh bilioni 250 na kuongeza kuwa
lengo ni kuwafanya Watanzania wengi kupata huduma ya afya kwa gharama
nafuu.
Alifafanua kwamba serikali imejenga barabara ya Kagoma-Biharamulo-
Lusahunga kwa gharama ya Sh bilioni 190, ambazo zote zimelipwa kutokana
na mapato ya ndani na kusema hayo ni mafanikio makubwa.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi tano za Afrika, zilizomudu
kujenga barabara kwa kutumia mapato yao wenyewe. Akasisitiza kwamba ni
muhimu miundombinu hiyo ikatunzwa. Rais aliwakumbusha Watanzania
kuendelea kutunza amani na utulivu uliopo.
Aliwataka wananchi kujifunza kutoka kwa baadhi ya nchi jirani, ambako
maelfu ya watu waliuawa kwenye migogoro ya wenyewe kwa wenyewe na hivyo
wasiruhusu mambo kama hayo kutokea nchini.
Alieleza kuwa serikali imeondoa kodi na ushuru kwenye mazao ili
kuwawezesha watu wa kipato cha chini kuwa huru. Alisema kwamba kodi hizo
ndizo zilizowashawishi watu kujiingiza kwenye biashara ya magendo na
nchi jirani ya mazao ikiwemo kahawa.
“Mkulima mwenye tani 20 za mazao ya chakula asikodi lori la tani 20
badala yake akodi tu lori la tani moja na hatatozwa kodi,” alisema Rais
Magufuli. Aidha, aliwahakikishia wakazi wa Biharamulo kwamba tatizo la
maji wanalokabiliana nalo, litatatuliwa hivi karibuni na kumwagiza
Mkurugenzi Mtendaji wa Maji Bukoba Mjini na Mamlaka ya Usafi (BUWASA),
Allen Marwa kuhakikisha mkandarasi aliyepewa kazi kufunga kuunganisha
mabomba kabla ya Julai 30, mwaka huu.
Aliwaagiza pia Mkuu wa Mkoa, Salum Kijuu na mkuu wa wilaya ya
Biharamulo, kuhakikisha mifugo inayozurura kwenye hifadhi za misitu
ukiwemo Burigi wanakamatwa. Rais Magufuli aliwataka Watanzania kuwa na
idadi ndogo ya mifugo, ambayo itawaingizia fedha na kuongeza kuwa
Tanzania bado haijanufaika vya kutosha kutoka sekta ya mifugo.
Pia aliwahakikishia wachimbaji wadogo wa Biharamulo kwamba serikali
itawapatia maeneo ya kuchimba dhahabu, inayopatikana katika eneo hilo.
Rais Magufuli yuko kwenye ziara ya siku mbili mkoani Kagera na leo
atakuwa wilayani Ngara, ambako pia atahutubia mkutano wa hadhara.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment