Home » » CHADEMA 51 WAREJEA URAIANI

CHADEMA 51 WAREJEA URAIANI


MAHAKAMA ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, imeamuru viongozi na wanachama 51 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuachiwa kwa dhamana.

Washtakiwa hao walikaa katika Gereza la Biharamulo mkoani Kagera kuanzia walipokamatwa Julai 7, mwaka huu.

Uamuzi huo umefanyika baada ya Mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi lililowekwa na upande wa mashtaka la kuwanyima dhamana viongozi hao na wanachama wa chama hicho kwenye kesi ya kufanya mkusanyiko bila kuwa na kibali.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu wa Mahakama hiyo, Jovith Kato, baada ya kupitia hoja za pande zote za Jamhuri na utetezi.

Awali upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Semen Nzigo, baada ya kuwafikisha mahakamani viongozi na wafuasi 51 wa Chadema kwa madai ya kufanya mkusanyiko pasipo kuwa na kibali kwenye kata ya Muganza wilayani hapa, uliweka pingamizi washtakiwa wasipewe dhamana kwa madai ya kutovurugwa kwa upelelezi wa kesi hiyo.

Hoja hiyo ilikubaliwa na mahakama, hivyo washtakiwa wote walipelekwa mahabusu kwenye Gereza la Biharamulo kabla ya mawakili wa upande wa utetezi kuiomba mahakama kuwaondolea zuio hilo.

Baada ya majibizano ya kisheria Jumatatu wiki hii upande wa Jamhuri na utetezi uliokuwa ukiongozwa na mawakili kutoka kampuni ya Goldbelt Advocates, John Edward na Siwale Isambi kukamilika, mahakama ilisubiriwa kutoa uamuzi.
 
Aidha, mawakili wa upande wa utetezi walitumia kifungu cha 148(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kupinga zuio lililowekwa na Jamhuri.

Akisoma uamuzi huo, hakimu Kato alisema baada ya kuzipitia hoja zote na kwa kina, mahakama imekubali ombi la upande wa utetezi kuwa kifungu namba 148(5) kilichowekwa na upande wa Jamhuri ili kuzuia dhamana ya washtakiwa hakiendani na zuio hilo.

Hakimu aliongeza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Ibara ya 13(6)(b) inatamka wazi kuwa ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.

Kadhalika Hakimu Kato alisema kwa mazoea ya uendeshaji wa mahakama katika mashauri ya jinai hayaliweki pingamizi hilo kuwa miongoni mwa makosa yanayonyima dhamana.

Kutokana na maelezo hayo, alisema washtakiwa wanayo haki ya kupewa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na wadhamini wawili kila moja na kwamba watatakiwa kuweka bondi ya Sh. 500,000 ndipo zitaandikwa hati za kuwafuata mahabusu kutoka katika Gereza la Biharamulo.

Wakati uamuzi huo unatolewa jana, washtakiwa hawakuletwa mahakamani. Aidha, Jumatatu hawakuletwa mahakamani.

Wakizungumzia hukumu hiyo nje ya mahakama, mawakili wa upande wa utetezi waliipongeza mahakama kwa kutenda haki, licha ya kwamba imetolewa kwa kuchelewa kutokana na wateja wao kusota mahabusu kwa siku 20.

Walisema baada ya uamuzi huo wa awali, wamejipanga vyema kuhakikisha wanapambana iwezekanavyo katika kesi ya msingi ambayo inadaiwa kuwa ya kukusanyika bila kibali ambayo itaanza baada ya polisi kukamilisha upelelezi.

Viongozi na wafuasi hao walikamatwa Julai 7 mwaka huu kwenye ukumbi wa Manzagata Kata ya Muganza wilayani Chato, wakiwa kwenye kikao cha ndani.

Baadhi ya viongozi walioko gerezani ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita, Phabian Mahenge, Katibu wa Chadema mkoa huo, Sudy Tuganyala, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee mkoa, Vitus Makoye na Mwenyekiti wa Bavicha mkoa huo, Neema Chozaile.

Wengine ni Katibu wa Wilaya ya Chato, Mange Ludomya, Kaimu Mwenyekiti Wilaya ya Chato, Uhuru Selemani, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa wilaya hiyo, Meshark Tulasheshe na Katibu Mwenezi Kata ya Muganza, Marko Maduka.
 Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa