Watu saba wamefariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Victoria eneo la hifadhi ya kisiwa cha Rubondo Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Ajali hiyo ilitokea Novemba 10, mwaka huu majira ya usiku wakati watu hao wakiwa katika shughuli za uvuvi jirani na eneo la hifadhi ya kisiwa cha Rubondo.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Diwani wa Kata ya Ikuza, Fortunatus Wazia, alisema kuwa watu hao walikuwa ni wavuvi kutoka sehemu mbalimbali za ndani na nje ya Wilaya ya Muleba.
Wazia alifafanua kuwa wavuvi hao walikumbwa na mkasa huo baada ya chombo walichokuwa wakisafiria kuzama.
Kwa mujibu wa diwani huyo, wavuvi hao walikwenda kuvua samaki kwenye kisiwa cha Rubondo kinyume cha sheria kwa kuwa ni eneo la hifadhi na boti hiyo ilizama kutokana na kutokuwa na ubora.
Alifafanua kuwa kutokana na hali hiyo, ilianza kuvuja maji wakati wakirejea kisiwani Ikuza kabla ya kuzama.
Kwa mujibu wa Wazia, watu hao waliondoka katika kisiwa cha Ikuza kwenda kwenye hifadhi ya Rubondo Novemba 8, mwaka huu na walipita njia za panya wakikwepa walinzi wa hifadhi wasiwakamate kwa kuwa walikuwa wanafanya ujangili.
Diwani huyo aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Baruya Masala, mkazi wa Muganza wilayani Chato; Alex Mwita, mkazi wa Tarime; Kipara Kasukari, mkazi wa Kata ya Mushabago wilayani Muleba na mwingine amejulikana kwa jina moja la Niko, mkazi wa Sengerema.
Wengine ni Obadia Yohana, mkazi wa Muganza; Juma Kengere, mkazi wa Itale Chato; na mwinge aliyetambuliwa kwa jina moja la Robert, mwenyeji wa Wilaya ya Biharamulo.
Wazia alisema kuwa baadhi ya miili ya marehemu hao ilitambuliwa na ndugu na jamaa zao na tayari ilimeshachukuliwa kwa ajili ya mazishi.
Hata hivyo, alisema maiti watatu hawakutambuliwa na ndugu mapema na kulazimika kuzikwa katika eneo la ufukweni mwa Ziwa Victoria katika kisiwa cha Ikuza wilayani Muleba.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Philip Kalangi, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na wavuvi hao kufariki dunia.
Kamanda Kalangi aliongeza kuwa Jeshi la Polisi mkoani Kagera linaendelea kuchunguza kwa lengo la kubaini chanzo cha ajali hiyo.