· Yana ukubwa ekari 7,700 katika vijiji viwili tu
· Aagiza Afisa Ardhi arudishwe kutoka Rorya kusaidia uchunguzi
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kufutwa mara moja umiliki wa mashamba
makubwa 11 yenye ukubwa wa ekari 7,700 kwenye vijiji vya Kasharazi na
Rwakalemera wilayani Ngara Kagera, ambayo hayana hati na yametelekezwa.
Ametoa
agizo hilo leo asubuhi (Jumatano, Machi 16, 2016) wakati akizungumza
na wakazi wa vijiji vya Kasulo na Rwakalemera katika kata ya Kasulo
wilayani Ngara akiwa njiani kuelekea mkoa wa Geita.
Waziri
Mkuu alilazimika kufanya mkutano huo mapema asubuhi baada ya kuamua
kuitisha uongozi wa wilaya ya Ngara ufike kwenye mkutano huo ili kujibu
kero za wananchi waliosimamisha msafara wake jana wakati akielekea Ngara
mjini.
Uamuzi
huo unafuatia hatua ya Waziri Mkuu kumwita kwenye mkutano huo Afisa
Ardhi na Maliasili wa Wilaya, Bi. Betty Munuo ili aeleze chanzo cha
mgogoro wa ardhi katika vijiji hivyo.
Bi.
Munuo ambaye amehamishiwa wilaya hiyo Agosti, mwaka jana, alisema
aliyakuta malalamiko hayo na amefanya uchambuzi wa majina ya wamiliki
wote wa mashamba na walikuwa wanapanga kuwapatia notisi ili wajieleze.
Katika
orodha yake, Bi. Munuo alitaja wamiliki 18 wa mashamba makubwa lakini
kati yao ni wamiliki saba tu ambao mashamba yao yana hati lakini matatu
ndiyo yameendelezwa na manne hayajaendelezwa.
Mashamba
yaliyoendelezwa yanatumika kwa kilimo, ufugaji na shule. Nayo
yanamilikiwa na Dayosisi ya Rulenge (shamba na. 606 lenye ekari 161 liko
Mbuba); Dario Zakaria (shamba na. 639 lenye ekari 282 liko Nyakariba)
na Masista wa Mt. Fransisco (shamba na. 234 lenye ekari 759 liko
Kasulo).
Mashamba
manne yenye hati lakini yametelekezwa ambayo yote yako kijiji cha
Rwakalemera ni ya Abdallah Sadala na. 235 lenye ekari 521; Mahsen Saidi
shamba na. 333 lenye ekari 458; Mshengezi Nyambele shamba na. 746 lenye
ekari 388 na Mushengezi Nyambele shamba na. 745 lenye ekari 497.
Akitangaza
uamuzi wake, Waziri Mkuu aliwataja wamiliki wa mashamba yasiyo na hati
kuwa ni Bw. Joseph Rugumyamheto mwenye shamba na. 527 (ekari 505 liko
Rwakalemera); Bw. Nicolaus Kidenke shamba halina namba na ukubwa wake
haujulikani; Bw. Gwasa Angas Sababili shamba na. 714 (ekari 236 liko
Kasharazi); na Bw. Makumi Adili Rufyega (ekari 500 liko Rwakalemera).
Wamiliki
wengine ambao mashamba yao yapo kijiji cha Rwakalemera ni Paulo Shikiri
ekari 250; Frank Mukama Derila ekari 750; Godfrey Kitanga ekari 800;
Philemon Mpanju ekari 200; Issa Sama ekari 500; Hekizayo Mtalitinya
ekari 225 na Joel Nkinga ekari 1,250.
Waziri
Mkuu aliagiza ifanyike sensa ili kubaini kama wamiliki wa mashamba hayo
yote ni Watanzania au la. "Haya yenye hati nataka yafanyike mapitio ya
hati zao na kubainisha ni namna gani walipatiwa hati hizo. Nataka
taarifa inifikie ofisini kwangu Dar es Salaam ifikapo tarehe 20 Machi,
2016," alisema.
Ili
kukamilisha kazi hiyo, Waziri Mkuu ameagiza kurejeshwa mara moja kwa
aliyekuwa Afisa Ardhi wa Wilaya hiyo, Bw. Enock Mponzi ambaye
amehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ili aje asaidie uchunguzi wa
ugawaji wa maeneo hayo.
Alimtaka
Mwenyekiti wa kijiji cha Rwakalemera, Bw. Brighton Kemikimba aitishe
mkutano wa kijiji kabla ya tarehe 31 Machi 2016 na abainishe mashamba
yote makubwa ambayo yanazidi ekari 50. Pia afuatilie kama yana kibali
cha Baraza la Madiwani.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu ameagiza kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Bw. Colnel Ngudungi na kutaka
arejeshwe wilayani humo kujibu tuhuma za kuhusika na upotevu wa fedha za
mauzo ya mbao kutoka kwenye msitu wa Rumasi, wilayani humo.
Kaimu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Adam Swai ameagizwa kumwandikia
barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga ili atekeleze maagizo hayo na
Bw. Ngudungi arejeshwe Ngara kujibu tuhuma hizo. Bw. Ngudungi
alihamishwa kwenda Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga, Agosti 2015.
Akiwa
njiani kuelekea Ngara jana mchana (Machi 15, 2016), waziri Mkuu
alisimamishwa katika kijiji cha Rwakalemera na wananchi wenye mabango
wakiomba kurejeshewa ardhi ya kijiji huku baadhi yao wakidai wanatishiwa
na bunduki pindi wakisogelea mashamba hayo makubwa.
Pia
walidai kuuzwa kwa msitu wa Rumasi na mapato kutojulikana yalipokwenda
huku wakidai kuwa kijiji chao hakipati mapato yoyote kutokana na minada
ya ng’ombe inayofayika kijijini hapo wakati sharia inataka asilimia 20
ya mapato ibakizwe kijijini.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, MACHI 16, 2016.