Home » » Mradi wa Umeme Vijijini (REA III) kufika Vijiji vyote nchini

Mradi wa Umeme Vijijini (REA III) kufika Vijiji vyote nchini


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kwikuba kuhusiana na Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akipokelewa na Mwenyekiti wa kijiji cha Kwikuba, Kamunyiro Kwibega.

Baadhi ya wananchi wakiagana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) mara baada ya kumaliza kuzungumza nao
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).
Serikali imesema vijiji vyote ambavyo havikufikishiwa huduma ya nishati ya umeme vitapata huduma hiyo kupitia Mradi mkubwa wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III).

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika ziara yake katika kijiji cha Kwikuba, Mkoani Mara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) ambao unamalizika.

Katika maeneo mbalimbali aliyotembelea Waziri Muhongo alielezwa kuwa vijiji vya ndani havina umeme kwani umeme umeishia kwenye vijiji vilivyopo katika barabara kubwa na kwenye senta za biashara.

Waziri Muhongo alisema Serikali inatambua vijiji ambavyo havikufikishiwa huduma husika na hivyo aliwaasa wananchi katika vijiji hivyo kuwa na subira kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha ndani ya miaka 10 vijiji vyote nchini view vimefikiwa na umeme.

Alisema Mradi huo wa REA III umetengewa zaidi ya trilioni moja ambayo ni mara tatu zaidi ya iliyotengwa kwa Mradi wa REA II ambao unamalizika kwa kuunganisha baadhi ya vijiji.

Aliongeza kuwa sasa hivi Serikali ipo katika utaratibu wa kuwapata Wakandarasi mahiri ambao watakabidhiwa jukumu la kutekeleza mradi huo ambao alisema ni mkubwa na wa kihistoria nchini.

Aidha akizungumzia mradi huo wa REA III, Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Amos Maganga alisema mbali na kuunganisha vijiji vyote, lakini pia mradi huo umelenga kuhakikisha unamaliza mapungufu yaliyojitokeza katika REA II.

Alisema katika utekelezaji wa mradi wa REA II kuna mapungufu yaliyojitokeza kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na wigo mpana na hivyo kusababisha baadhi ya vijiji kurukwa na vingine kutofikiwa kabisa na vilevile uhaba wa baadhi ya vifaa katika maeneo mbalimbali.

Aliwaasa wananchi ambao vijiji vyao havijafikishiwa huduma ya nishati ya umeme kuwa na subira kwani mradi mkubwa wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) hautaacha kijiji.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa