Dk. Faustine Ndungulile Kulia Akiongea na Mzee Mmojawapo Anaishi Katika Kituo cha Wazee Kiilima
Naibu Waziri wa Afya Dk. Faustine Ndungulile Akionesha Mfano wa Kufyatua Tofali Ili Nyumba za Watumishi Zijengwe Katika Kituo cha Wazee Kiilima
Mkuu wa Mkoa Kagera Mhe. Kijuu (Kulia) Akipokea Ahadi ya Vifaa Vilivyohaidiwa na Redcross Wakati wa Harambee Mabati 20, Blanketi 20 na Vyandarua
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu Aliyesimama Kulia Akitoa Taarifa kwa Naibu Waziri wa Afya Dk. Ndungulile
Naibu Waziri wa Afya Dk. Faustine Ndungulile Akionesha Mfano wa Kufyatua Tofali Ili Nyumba za Watumishi Zijengwe Katika Kituo cha Wazee Kiilima
Nyumba za Watumishi (Kulia) Zinazotakiwa Kujengwa Upya Kwasababu ya Uchakavu Katika Kituo cha Wazee Kiilima Zikikaguliwa na Waziri Ummy Mwalimu
Na:
Sylvester Raphael
Naibu Waziri wa Afya , Maendeleo
ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dk.
Faustine Ndungulile afanikisha kupatikana
kwa zaidi ya shilingi milioni 17 kwenye
harambee ya kuchangia ujenzi wa Nyumba ya
Watumishi katika Kituo cha Wazee Kiilima Kata ya Nyakato Wilayani Bukoba Mkoani
Kagera.
Katika Harambee hiyo iliyofanyika
Februari 22, 2018 katika Kituo cha Wazee Kiilima Dk. Ndungulile akiwa Mgeni Rasmi alichangisha fedha taslimu milioni
7,000,000/= na kiasi cha shilingi milioni 11 zikiwa ahadi kutoka kwa wadau
mbalimbali pamoja ahadi za vifaa kama magodoro, saruji, baiskeli za wazee na mabati.
Katika hotuba yake kwa wananchi
na wadau mbalimbali waliohudhuria harambee hiyo Naibu Waziri Dk. Ndungulile
aliwasisitiza wananchi kuwa na moyo wa kujitolea kuchangia kituo hicho ili
watumishi wanaowatunza wazee wapate mazingira mazuri ya kuishi baada ya kufanya
kazi yao ya kuwahudumia wazee hao.
“Serikali itaendelea kuwaunga mkono wananchi kwa kuleta fedha katika kituo
hiki ili kikamilike ujenzi wake na Wazee wetu
waweze kuhudumiwa na watumishi ambao watawaza ni wapi pa kuishi au kukaa
salama mara baada ya kufanya kazi yao ya kuwahudumia Wazee wetu,” Alisisitiza
Dk. Ndungulile.
Kituo cha Kutunza Wazee Kiilima
ni kituo cha Serikali kilichopo chini ya Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto. Kituo Hicho kilijengwa upya na Serikali baada
ya kuathiriwa na Tetemeko la Ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 Mkoani Kagera.
Majengo yaliyojengwa upya na
Serikali ni pamoja na Mabweni mawili ya Wanaume na Wanawake, Jiko, stoo ya
kutunzia chakula, Sehemu ya kulia chakula, sehemu ya kupumzikia wazee, vyoo viwili vya wanawake na wanaume.
Changamoto iliyokuwa imebaki ni nyumba za watumishi ambazo kwa sasa zina hali
mbaya ya uchakavu na hazistahili tena kuishi watu.
Fedha zilizopatikana zinatarajiwa
kujenga nyumba mbili za watumishi (Two in One) ili kutatua changamoto ya
watumishi wanaoishi na kufanya kazi ya kuwahudumia wazee ili wapate mahali
salama pa kuishi na kutimiza wajibu wao kikamilifu bila kuwa na changamoto za
sehemu za kuishi.
Katika Hatua nyingine Naibu Waziri Dk. Ndungulile alimshukuru Mkuu
wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu kwa juhudi zake za
kuipatia Bohari ya Dawa (MSD) kiwanja
cha kujenga Bohari ya dawa katika Manispaa ya Bukoba na Mkoani Kagera ili
kurahisisha upatikanaji wa dawa zote hapa Kagera.
Pia Dk. Ndungulile alimuomba Mkuu
wa Mkoa kuhamasisha wananchi kuitikia wito wa kuwapeleka watoto wa kike miaka 4
hadi 9 kwenda kwenye vituo vitakavyokuwa vimepangwa kupata chanjo ya kansa ya
shingo na uzazi kwani imeonekana kuwa kuna ongezeko kubwa la Kansa ya Shingo na
uzazi katika mkoa wa Kagera.
Akimshukuru Naibu Waziri kwa
kuamua kufanya ziara ya kukagua shughuli za afya Mkoani Kagera Mkuu wa Mkoa
Kijuu aliomba Wizara ya Afya kuangalia upya tatizo la ugonjwa wa Malaria katika
Mkoa wa Kagera kwani pamoja na juhudi zote zinazofanyika laikini kiwango cha
ugonjwa huo kinazidi kupanda ambapo Naibu Waziri Dk. Ndungulile alisema tayari
Wizara imeliona hilo na linafanyiwa kazi.
Naibu Waziri Dk. Ndungulile akiwa
Mkoani hapa katika ziara yake ya siku mbili alivitembelea pia vituo vya Afya Kabyaile
Wilayani Missenyi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Kituo cha Afya Kaigara
na Kituo cha Afya Kimeya Wilayani Muleba ili kukagua huduma za Afya
zinavyotolewa kwa wananchi na kuongea na watumishi katika maeneo hayo.