Dar es Salaam. Mvua kubwa isiyotabirika inatarajiwa kunyesha katika
maeneo mbalimbali nchini hasa katika ukanda wa Pwani ya Kaskazini,
maeneo ya Dar es Salaam, Tanga, Unguja na Pemba; pia katika ukanda wa
Kaskazini Mashariki kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Akitoa taarifa ya hali ya hewa jana kwa Januari na Februari mwaka ujao,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agness
Kijazi alisema mvua ya msimu katika maeneo hayo inatarajiwa kwisha leo.
Hata hivyo, alisema mvua kubwa ya nje ya msimu inatarajiwa katika
kipindi cha Januari, 2015. Dk Kijazi alisema hali kama hiyo pia
itaikumba mikoa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga na Geita.
“Maeneo mengine yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka yatakuwa na
mvua ya wastani. Maeneo hayo ni Mbeya, Rukwa, Katavi, Iringa, Lindi,
Dodoma na Mtwara.
Dk Kijazi alisema mvua hiyo inasababishwa na ongezeko la joto
linalolifanya anga kushindwa kutengeneza unyevunyevu ambao hugeuka kuwa
mvua. “Ninawashauri wananchi kuchukua hatua ya kujikinga na athari za
kiafya na mazingira zinazoweza kusababishwa na ongezeko la joto
linaloendelea sambamba na mvua kubwa inayonyesha,” alisema Dk Kijazi.
Juzi, mvua kubwa ilinyesha jijini Dar es Salaam kwa saa mbili na
kusababisha vifo vya watu wawili katika Wilaya ya Kinondoni kuleta kero
kwa wasafiri wanaotumia vyombo vya moto na watembea kwa miguu.
Mitaa ya Azikiwe, Bibi Titi na Morogoro ambayo juzi ilijaa maji, jana ilionekana kuwa mikavu baada ya maji yote kukauka.
huku watumiaji wa barabara wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.
Yusuph Said, mmoja wa wafanyabiashara wa magezeti Mtaa wa Azikiwe,
alisema eneo hilo hujaa maji kila mvua inaponyesha na kuwasababishi
kufanya kazi yao katika mazingira magumu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura aliliambia gazeti
hili jana kuwa hakuna madhara zaidi yaliyotokea ukiacha matukio ya watu
wawili kufariki dunia kutokana na mvua hiyo.
Naye Kamanda wa Polisi Ilala, Mary Nzuki alisema: “Mkoani kwangu
sijapokea taarifa yoyote ya maafa yaliyosababishwa na mvua mpaka sasa.”
Kamanda Kihenya Kihenya wa Mkoa wa Kipolisi Temeke naye alisema
hajapokea taarifa yoyote ya maafa.
Akizungumzia matukio ya mvua kipindi cha Oktoba – Disemba, 2014, Dk
Kijazi alisema maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za wastani hadi juu ya
wastani isipokuwa maeneo machache ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam,
Dodoma (Hombolo), Kilimanjaro (Same), Njombe, Mtwara na Lindi ambayo
yalipata mvua za chini ya wastani.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa matukio ya mvua hizo ambayo yaliambatana
na vipindi vifupi vya upepo mkali, yalisababishwa na kuimarika kwa
ukandawa mvua magharibi mwa nchi ambao uliambatana na kuwepo kwa
makutano ya upepo.
“Wananchi wajenge pia utamaduni wa kupanda miti ili kusaidia kupunguza
kasi ya upepo unaombatana na mvua kubwa ambazo zinaweza kusababisha
uharibifu wa mali na madhara kwao,” alisisitiza Dk Kijazi.
Peter Elias, Bakari kiango na Hadija Salum wa Mwananchi