Home » » HALMASHAURI ZAAGIZWA KUHAKIKI WAKANDARASI

HALMASHAURI ZAAGIZWA KUHAKIKI WAKANDARASI

HALMASHAURI za wilaya zimeagizwa kuunda kamati ndogo kwa ajili kuhakiki wakandarasi waliopewa zabuni za kutengeneza barabara.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Enosi Mfuru, katika kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika Manispaaa ya Bukoba.

Alisema uhakiki na ukaguzi huo utasaidia kuondoa tatizo la wakandarasi kujenga barabara chini ya kiwango na kulipwa fedha, hali inayochangia kuzisababishia hasara halmashauri na serikali kwa ujumla.

Mfuru alisema ukaguzi huo utasaidia kupunguza malalamiko yaliyoanza kujitokeza kuwa baadhi ya barabara zinatengenezwa chini ya viwango na kusababisha kushindwa kupitika muda mfupi baada ya kutengenezwa.

“Halmashauri zihakikishe kila kijiji kinaweka ulinzi katika barabara hilo, ili kuweza kuzilinda hasa zile za Stabex zilizokuwa zinahudumiwa na jumuiya hiyo kutoka Ulaya, kwani mkataba wake umekwisha zitunzwe kama zamani kabla ya msaada huo,” alisema Mfuru.
Aliwakataza wale ambao wameanza kuchimba madini karibu na barabara hizo, kwani wamekuwa wakisababisha uharibifu wa barabara na kuwataka watafute sehemu nyingine.

Meneja wa TanRoads mkoani hapa, Jonh Kalupale, alisema jumla ya sh bilioni 6 ziliidhinishwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara kuu za mkoa katika mwaka wa fedha 2008/09. Kati ya hizo sh bilioni 3.6 ni kwa ajili ya kuhudumia barabara kuu zenye urefu wa kilomita 468.62 na madaraja 126.

Aidha, Kalupale alikiomba kikao hicho kwa kupitia kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kuwawekea ulinzi wa kutosha makandarasi wanaofanya kazi katika mapori ya Burigi Kasindaga na Kimisi, ili kulinda mali zao na usalama wao kwa ujumla 
 Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa