Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Bukoba, limewasimamisha
watumishi wanane kutokana na ufisadi wa Sh milioni 851 zilizotolewa na
Serikali pamoja na wafadhili kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella ameagiza kuchukuliwa
hatua za kijinai kwa watendaji wote waliohusika. Mongella alishtushwa na
taarifa ya tume iliyoundwa na uongozi wa mkoa huo kuchunguza matumizi
ya fedha hizo kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo limekaa
kikao cha dharura na kuwasimamisha watumishi hao ili kupisha uchunguzi.
Waliosimamishwa ni aliyekuwa Mganga Mkuu (DMO), Hamza Mgula kabla ya
kuhamishiwa Manispaa ya Bukoba, Idara ya Fedha ni Mweka Hazina, Jonathan
Katunzi na Selialisi Mtalemwa, Kitengo cha Ujenzi; Robert Massoro na
Deus Bizibu, Ofisa Mipango na Ofisa Elimu Sekondari, Lucas Mzungu, Idara
ya Mipango, Mustapha Sabuni na Idara ya Mifugo, Dk Kisanga Makigo.
Hali hiyo ilikuja wakati Mwenyekiti wa Tume ya watu sita, Wambura
Sabora kutoa taarifa katika kikao maalumu cha madiwani, watumishi wa
halmashauri hiyo, wakuu wa idara kutoka mkoani na mkuu huyo wa mkoa juu
ya waliyobaini ndani ya siku nne walizofanya ukaguzi na uchunguzi ambapo
walidai kubaini madudu.
“Katika uchunguzi tulibaini kuwa fedha kutoka Basket Fund milioni 307
zilizotolewa na Serikali 2011/2012 kwa ajili ya kununulia dawa katika
hospitali na vituo vya afya zilihamishwa na kutumika tofauti na malengo
bila kufuata taratibu zinazostahili huku milioni 200 za Mfuko wa
Barabara zilizotolewa 2014 kwa ombi maalumu ambazo zilizotolea kwa mfumo
wa kibajeti hazikutumika kama ilivyokusudiwa na badala yake
zilihamishiwa sehemu nyingine ikiwemo matumzi ya ofisi,” Wambura
alisema.
Alitaja fedha nyingine kuwa ni Sh milioni 168 za Mfuko wa Jimbo
ambazo pia zimetumika katika shughuli nyingine, bila idhini ya kikao
chochote wala nyaraka inayoonesha kuhamishwa kwa fedha hiyo jambo ambalo
ni kosa kisheria kwani ni matumizi yanayotia shaka.
Baada ya Mkuu wa Mkoa kupata taarifa hiyo, aliwataka Mweka Hazina,
John Katunzi kutoa maelezo, na akakiri kuwepo kwa upungufu huo huku
akibainisha walibadilisha matumizi ya fedha hiyo baada ya kukaa na
Mkurugenzi wakati huo Glades Ndyamvunye.
Inaelezwa kuwa walipanga kurudisha fedha hizo lakini hadi sasa
hazijarudishwa. Pamoja na hayo, alimwagiza Mkuu wa Taasisi ya Kupambana
na Kuzuia Rushwa (Takukuru) Mkoa, Joseph Mwaiswelo na Kamanda wa Polisi
wa Mkoa huo kuwachukulia hatua zaidi watuhumiwa kwa yale yatakayobainika
kuwa ya kijinai.
CHANZO ; HABARI LEO.