SERIKALI mkoani Kagera imemtaka mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Colnery Ngudungi kuhakikisha halmashauri hiyo inashinda kesi inayohusu upotevu wa kiasi cha Sh milioni 30.
Fedha hizo ni sehemu ya Sh milioni 150 zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya mradi wa maji Kibimba wilayani humo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera John Mongella, alipofanya ziara katika eneo la mradi huo unaojengwa kwa ajili ya matumizi ya maji kwa wananchi wa mji mdogo wa Ngara ikiwemo hospitali teule ya wilaya iitwayo Mulugwanza.
Alitoa kauli hiyo baada ya kupata taarifa kwamba kuna mradi wa maji ambao fedha yake ilitolewa na Rais Kikwete, lakini kuna watu wameuhujumu.
Kutokana na taarifa hiyo, RC huyo aliamua kwenda kukagua mradi huo na kujionea maendeleo yake, ikiwa ni sambamba na kupata maelezo kutoka kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo Ngudungi.
Mkurugenzi alitoa maelezo kwa mkuu huyo wa mkoa ambapo alisema halmashauri hiyo iliomba kiasi cha Sh milioni 200 kwa ajili ya kuboresha miundombimu ya maji mjini Ngara na Rais Kikwete alipofanya ziara wilayani humo mwezi Julai mwaka jana aliahidi kuchangia mradi huo kiasi cha Sh milioni 150.
Alisema Rais alituma kwanza kiasi cha Sh milioni 50 na mara ya pili ilitolewa Sh milioni 100. Alisema fedha hiyo ilitumwa kupitia akaunti ya mamlaka ya maji Ngara jambo lililompa mwanya aliyekuwa Meneja wa mamlaka hiyo, Edward Magai kujichotea kiasi cha Sh milioni 32.
Alisema ili mradi huo ukamilike una unahitaji Sh milioni 43 na baraza la madiwani limeishakaa vikao na kuazimia kuwa hizo fedha zipatikane na kumalizia mradi huo ili kupunguza adha ya ukosefu wa maji katika mji huo ambao wananchi hufuata maji zaidi ya kilometa saba.
Kutokana na maelezo hayo mkuu wa mkoa alitoa agizo halmashauri itafute fedha hizo ili mradi ukamilike lakini pia akaagiza kuhakikisha kesi iliyoko mahakamani halmashauri inashinda.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment