Mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewataka viongozi na makada
wengine waliobaki ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoroka na
kujiunga na Chadema kwani hivi sasa ni wakati wa mabadiliko.
Lowassa alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Soko jipya wilayani Biharamulo, Mkoa wa Kagera.
Lowassa alisema huu ni wakati wa mabadiliko, hivyo aliwaomba viongozi wengine ambao bado wamo ndani ya CCM kujiunga na Chadema.
“Kama viongozi wengine bado wapo CCM wanataka kuja Chadema waje ili tuungane katika safari hii ya mabadiliko,” alisema.
Aidha, alimpongeza Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu, kwa uamuzi wake wa kujiondoa CCM
na kujiunga na wana-mabadiliko.
Akizungumzia walimu, Lowassa alisema akiingia madarakani hatataka kusikia mishahara na posho za walimu zinachelewesha.
Lowassa alisema akiingia madarakani atahakikisha walimu wanalipwa vizuri ili wawape wanafunzi elimu bora.
“Sitaki kusikia kuna mizengwe mizengwe ya walimu kucheleweshewa mishahara au posho,” alisema Lowassa.
Aidha, mgombea huyo alisema akiingia madarakani atahakikisha Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT) linaanzisha vyuo vya Elimu ya Ufundi Stadi (Veta)
ili vijana wanapomaliza mafunzo wanatoka na utaalamu.
“Nataka ndani ya JKT kuwe na vyuo vya ufundi vya kufundisha watu
kutengeneza pikipiki, baiskeli hata na magari. Nina imani kwa miaka
mitano tutapata wataalamu wazuri,” alisema.
Aidha, alimpongeza Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, kwa kuijenga Chadema, akisema imekuwa imara na yenye nguvu.
Kabla ya kuwahutubia wananchi, Lowassa aliwaomba watulie kwa dakika
kadhaa kwa ajili ya kumkumbuka Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Nyerere, ambaye jana Watanzania waliadhimisha kumbukumbu ya miaka 16 ya
kifo chake.
MBOWE
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, alisema ilani ya Chadema imeeleza mambo ya msingi ambayo serikali ya Lowassa itayatekeleza.
“Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kilikuwa ni kilio cha Chadema
cha kuwa na katiba ambayo itawawajibisha viongozi na kusimamia
rasilimali za nchi,” alisema.
Hata hivyo, alisema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilipiga vita
rasimu ya katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ambayo ilitokana na maoni ya wananchi.
Aidha, alisema ujio wa Lowassa, Kingunge Ngombale Mwiru na na
Frederick Sumaye imekuwa ni baraka kwa Chadema na Watanzania kwa ujumla.
KINGUNGE
Kwa upande wake muasisi wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, alisema
huu ni wakati muhimu kwa Watanzania wote kutambua kuwa muda wa kufanya
mabadiliko umefika.
“Nusu karne imetosha na kwa bahati nzuri uongozi wa sasa wa CCM
umeishiwa pumzi, hauwezi kuwaongoza Watanzania tena,” alisema na
kuongeza:
“Ndiyo maana Lowassa ameondoka, Sumaye ameondoka na mimi Kingunge
ambaye hakuna mwingine zaidi yangu nimeondoka CCM, huu ni wakati wa
kuiweka CCM benchi.”
MASHA
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, alisema
CCM ingeweza kufanya vizuri kama si ufisadi uliopo ndani ya chama hicho
ambao unasababisha wapatikane viongozi wasiofaa.
“Kinana (Adrulrahman), ndiye wa kwanza kuwaeleza wananchi kuhusu
mawaziri mizigo na yeye ndiye anazunguka nchi nzima kukikosoa chama
chake,” alisema na kuongeza:
“Haya mwisho wake ni Oktoba 25, mwaka huu...ingawa katika kipindi
hiki watu wanaweza kuonewa na wengine kuambiwa si raia, lakini lazima
yafike mwisho.”
Aidha, aliwataka wananchi kutii sheria na kuliheshimu Jeshi la Polisi katika kipindi hiki.
“Naomba nyie polisi mkumbuke kuwa na nyinyi ni Watanzania,
tunafahamu mpo hapa kwa ajili ya kulinda amani, lakini tunaomba mtumie
busara na hekima pia,” alisema Masha.
Jana Lowassa alihutubia mikutano ya kampeni katika maeneo ya Biharamulo, Ngara Mjini na Vijijini pamoja na Mbogwe.
MBOWE AMJIBU JK
Akiwa katika mkutano wa jana jioni uliofanyika Mbogwe, wilayani
Geita, Mbowe alimtaka Rais Kikwete kutovuruga amani ya nchi na badala
yake aondoke salama.
Alisema Rais Kikwete aondoke madarakani salama kama walivyofanya marais wenzake wastaafu.
“Rais Kikwete ameamua kuwa mpiga debe wa Magufuli (mgombea wa CCM),
sasa mimi naomba nimjibu yeye kama mpiga debe na si rais,” alisema.
Alisema Rais Kikwete ameamua kuwaaminisha Watanzania kuwa wapiga
kura wapo milioni 28 badala ya milioni 22 kama ilivyotangazwa na Tume ya
Taifa ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
“Sasa nataka kumuuliza Rais Kikwete hao wapiga kura wengine milioni sita wametoka wapi?” alihoji Mbowe na kuongeza:
“Naomba kumwambia Rais Kikwete kuwa hii nchi si yake, hii nchi si
ya CCM na hii nchi si ya familia yake...hii ni nchi ya Watanzania,”
alisema.
Alisema hatua ya Rais Kikwete na CCM inayoungwa mkono na Nec
kuwataka wananchi wapige kura na kuondoka vituoni haiwatendei haki
Watanzania.
“Kikatiba Watanzania wana haki ya kulinda kura zao kwa sababu zile
ni kura zao, nashangaa Rais Kikwete anawaambia watu waondoke,” alisema.
Mbowe, aliwaomba Watanzania wote kwenda kwenye vituo kwa ajili ya kupiga kura ikiwa ni pamoja na kuzilinda kura zao.
Pia alisema anashangazwa na kauli ya Rais Kikwete ya kuliagiza
Jeshi la Polisi kuwaondoa wananchi kwa nguvu katika vituo vya kupigia
kura.
“Hao askari walioagizwa na Rais Kikwete, nao wana watoto na familia
zao, naomba nikwambie Rais Kikwete kuwa huwezi kuzuia mabadiliko.
Zimebaki siku 11, Mungu atajibu maombi yetu...nawaambia wananchi nendeni
mkapige kura kaeni mita 200 lindeni kura zetu,” alisema.