Home » » Lowassa: Mliobaki CCM sasa nifuateni Chadema.

Lowassa: Mliobaki CCM sasa nifuateni Chadema.

Mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Na Jacqueline Massano
Mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewataka viongozi na makada wengine waliobaki ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoroka na kujiunga na Chadema kwani hivi sasa ni wakati wa mabadiliko.
 
Lowassa alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Soko jipya wilayani Biharamulo, Mkoa wa Kagera.
 
Lowassa alisema huu ni wakati wa mabadiliko, hivyo aliwaomba viongozi wengine ambao bado wamo ndani ya CCM kujiunga na Chadema.
 
“Kama viongozi wengine bado wapo CCM wanataka kuja Chadema waje ili tuungane katika safari hii ya mabadiliko,” alisema.
 
Aidha, alimpongeza Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu, kwa uamuzi wake wa kujiondoa CCM na kujiunga na wana-mabadiliko. 
 
Akizungumzia walimu, Lowassa alisema akiingia madarakani hatataka kusikia mishahara na posho za walimu zinachelewesha.
 
Lowassa alisema akiingia madarakani atahakikisha walimu wanalipwa vizuri ili wawape wanafunzi elimu bora.
 
“Sitaki kusikia kuna mizengwe mizengwe ya walimu kucheleweshewa mishahara au posho,” alisema Lowassa.
 
Aidha, mgombea huyo alisema akiingia madarakani atahakikisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linaanzisha vyuo vya Elimu ya Ufundi Stadi (Veta) ili vijana wanapomaliza mafunzo wanatoka na utaalamu.
 
“Nataka ndani ya JKT kuwe na vyuo vya ufundi vya kufundisha watu kutengeneza pikipiki, baiskeli hata na magari. Nina imani kwa miaka mitano tutapata wataalamu wazuri,” alisema.
 
Aidha, alimpongeza Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, kwa kuijenga Chadema, akisema imekuwa imara na yenye nguvu.
 
Kabla ya kuwahutubia wananchi, Lowassa aliwaomba watulie kwa dakika kadhaa kwa ajili ya kumkumbuka Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye jana Watanzania waliadhimisha kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo chake.
 
MBOWE
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, alisema ilani ya Chadema imeeleza mambo ya msingi ambayo serikali ya Lowassa itayatekeleza. 
 
“Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kilikuwa ni kilio cha Chadema cha kuwa na katiba ambayo itawawajibisha viongozi na kusimamia rasilimali za nchi,” alisema.
 
Hata hivyo, alisema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilipiga vita rasimu ya katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilitokana na maoni ya wananchi. 
 
Aidha, alisema ujio wa Lowassa, Kingunge Ngombale Mwiru na na Frederick Sumaye imekuwa ni baraka kwa Chadema na Watanzania kwa ujumla.
 
KINGUNGE
Kwa upande wake muasisi wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, alisema huu ni wakati muhimu kwa Watanzania wote kutambua kuwa muda wa kufanya mabadiliko umefika.
 
“Nusu karne imetosha na kwa bahati nzuri uongozi wa sasa wa CCM umeishiwa pumzi, hauwezi kuwaongoza Watanzania tena,” alisema na kuongeza:
 
“Ndiyo maana Lowassa ameondoka, Sumaye ameondoka na mimi Kingunge ambaye hakuna mwingine zaidi yangu nimeondoka CCM, huu ni wakati wa kuiweka CCM benchi.”
 
MASHA
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, alisema CCM ingeweza kufanya vizuri kama si ufisadi uliopo ndani ya chama hicho ambao unasababisha wapatikane viongozi wasiofaa.
 
“Kinana (Adrulrahman), ndiye wa kwanza kuwaeleza wananchi kuhusu mawaziri mizigo na yeye ndiye anazunguka nchi nzima kukikosoa chama chake,” alisema na kuongeza:
 
“Haya mwisho wake ni Oktoba 25, mwaka huu...ingawa katika kipindi hiki watu wanaweza kuonewa na wengine kuambiwa si raia, lakini lazima yafike mwisho.”
 
Aidha, aliwataka wananchi kutii sheria na kuliheshimu Jeshi la Polisi katika kipindi hiki.
 
“Naomba nyie polisi mkumbuke kuwa na nyinyi ni Watanzania, tunafahamu mpo hapa kwa ajili ya kulinda amani, lakini tunaomba mtumie busara na hekima pia,” alisema Masha.
 
Jana Lowassa alihutubia mikutano ya kampeni katika maeneo ya Biharamulo, Ngara Mjini na Vijijini pamoja na Mbogwe.
 
MBOWE AMJIBU JK
Akiwa katika mkutano wa jana jioni uliofanyika Mbogwe, wilayani Geita, Mbowe alimtaka Rais Kikwete kutovuruga amani ya nchi na badala yake aondoke salama.
 
Alisema Rais Kikwete aondoke madarakani salama kama walivyofanya marais wenzake wastaafu.
 
“Rais Kikwete ameamua kuwa mpiga debe wa Magufuli (mgombea wa CCM), sasa mimi naomba nimjibu yeye kama mpiga debe na si rais,” alisema.
 
Alisema Rais Kikwete ameamua kuwaaminisha  Watanzania kuwa wapiga kura wapo milioni 28 badala ya milioni 22 kama ilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
 
“Sasa nataka kumuuliza Rais Kikwete hao wapiga kura wengine milioni sita wametoka wapi?” alihoji Mbowe na kuongeza:
 
“Naomba kumwambia Rais Kikwete kuwa hii nchi si yake, hii nchi si ya CCM na hii nchi si ya familia yake...hii ni nchi ya Watanzania,” alisema.
 
Alisema hatua ya Rais Kikwete na CCM inayoungwa mkono na Nec kuwataka wananchi wapige kura na kuondoka vituoni haiwatendei haki Watanzania.
 
“Kikatiba Watanzania wana haki ya kulinda kura zao kwa sababu zile ni kura zao, nashangaa Rais Kikwete anawaambia watu waondoke,” alisema.
 
Mbowe, aliwaomba Watanzania wote kwenda kwenye vituo kwa ajili ya kupiga kura ikiwa ni pamoja na kuzilinda kura zao.
 
Pia alisema anashangazwa na kauli ya Rais Kikwete ya kuliagiza Jeshi la Polisi kuwaondoa wananchi kwa nguvu katika vituo vya kupigia kura.
 
“Hao askari walioagizwa na Rais Kikwete, nao wana watoto na familia zao, naomba nikwambie Rais Kikwete kuwa huwezi kuzuia mabadiliko. Zimebaki siku 11, Mungu atajibu maombi yetu...nawaambia wananchi nendeni mkapige kura kaeni mita 200 lindeni kura zetu,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa