Home »
» ZITTO: HERI NIWE MSALITI WA CHAMA SI TAIFA
ZITTO: HERI NIWE MSALITI WA CHAMA SI TAIFA
KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Bw. Zitto Kabwe, amesema ni heri aendelee kuitwa msaliti na watu wasio na dhamira nzuri ya kupigania masilahi ya nchi kuliko kuwasaliti wananchi.
Alisema ataendelea na msimamo wa kuhakikisha masilahi ya Taifa yanawekwa mbele badala ya kukubali kukumbatiwa na watu wenye dhamira ya kunufaisha matumbo na familia zao.
Bw. Kabwe aliyasema hayo Mjini Bukoba, mkoani Kagera juzi kwenye mkutano wa hadhara ikiwa ni mara yake ya kwanza kuwahutubia wakazi wa mji huo tangu aingie kwenye siasa.
Aliongeza kuwa, kabla ya kufumuka mgogoro katika chama chake cha zamani (CHADEMA), wapinzani walikubaliana masuala mbalimbali ya kusimamia likiwemo la kukataa kuchukua posho za vikao, kutotumia mali za umma kwa manufaa ya chama.
Alisema dhamira ya makubaliano hayo ni kuibana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa inapotaka kusamehe kodi kiholela, kutumia mali za umma kwa masuala yao ya chama na kujipatia posho zisizo na sababu.
"Ndugu zangu wana Bukoba, kilichoniponza ni kusimamia masilahi ya umma si kingine, nilitaka tujitofautishe na CCM lakini wenzangu hawakuwa tayari, kama wote tunachukua posho, kama wote hatutaki kufutiwa msamaha wa kodi na kutumia mali za umma kwa ajili ya vyama vyetu, tofauti yetu itakuwa nini na chama tawala," alihoji Bw. Kabwe.
Aliongeza kuwa, wote wanaomuita msaliti wanapaswa kuwaeleza wananchi wamewafanyia nini ili kutimiza majukumu yao ya kibunge muda wote waliokuwa bungeni.
Alisema kamwe ACT-Wazalendo hakitapita katika makosa ambayo yamefanywa na vyama vingine na kukubaliana kuzindua Azimio la Tabora kutoka katika mazuri ya Azimio la Arusha.
Bw. Kabwe alisema jambo lingine ambalo aliliweka wazi wakati akiwa mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ni kutaka vyama vya siasa vikaguliwe hesabu zao kwa kuwa vinapokea ruzuku ya Serikali ambayo ni kodi ya wananchi.
"Katika kulitetea Taifa, mimi nilionekana msaliti kwa sababu nilipigania masilahi ya wananchi ambao bado wana kipato cha chini, nipo tayari kuitumikia nchi si kukitumikia chama kwani chama kinapita," alisema Zitto na kuongeza;
"Fedha hizi lazima zikaguliwe ili ifahamike matumizi halali si vinginevyo, nilipokuwa Mwenyekiti wa PAC, nilisema lazima ukaguzi ufanyike kwa vyama vyote kwani hapa tunatetea masilahi ya umma," alisema.
Aliongeza kuwa, Taifa la Tanzania ni la wananchi ambao wengi wao ni maskini; hivyo wanahitaji kuwa na kiongozi jasiri mwenye uthubutu wa kufanya yale anayohubiri hadharani.
Aliongeza kuwa, Tanzania inahitaji mabadiliko na chama cha ACT-Wazalendo kimeanza kutekeleza kwa kuzindua Azimio
la Tabora ambalo limehuishwa kutoka Azimio la Arusha.
Bw. Kabwe alifafanua kuwa, kiongozi yeyote wa chama hicho ambaye atachaguliwa kwenye nafasi ya kiserikali, hatapokea posho za vikao wakiwemo wabunge kwani vikao vya Bunge ni sehemu ya kazi zao.
Alisema hivi sasa nchi imekithiri kwa rushwa na ufisadi mkubwa kutokana na kundi la watu wachache walio wafanyabiashara na wanasiasa.
"Hata watia nia wa nafasi ya urais waliojitokeza hadi sasa katika vyama mbalimbali, wengi wao hawana dhamira ya kupambana na rushwa kwa kuwa wengi wao ni wala rushwa na mafisadi wakubwa.
"Wakati wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, si kwamba hakukuwa na rushwa ilikuwapo ndogo ndiyo maana Mwalimu aliweka miiko
na maadili ya viongozi kwa kufuata Azimio la Arusha, hivi sasa nchi haipo katika rushwa; bali ufisadi hali ambayo ni hatari kwa Taifa letu," alisema Bw. Kabwe.
0 comments:
Post a Comment