SERIKALI wilayani Missenyi mkoani Kagera imetoa siku 14 kwa wamiliki
wa ng’ombe 240 waliokamatwa ndani ya ranchi ya Missenyi, Machi mwaka
huu, kulipa faini na kukomboa mifugo yao, vinginevyo Serikali itaiuza
kwa mnada.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo jana , Festo Kiswaga
alipofanya mkutano na wafugaji ambao pia ni wamiliki wa mifugo hiyo
katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri mjini hapa .
Agizo hilo la Kiswaga amelitoa kutokana na mifugo hiyo kuendelea
kushikiliwa kwa muda mrefu toka Machi mwaka huu huku wamiliki wake
wakiweka msimamo wa kupinga utaratibu wa kuwachukua kwa kulipa faini.
“Taarifa niliyo nayo ni kwamba Machi mwaka huu, ng’ombe hao waliingia
kinyemela katika Ranchi ya Missenyi huku baadhi yao wakidaiwa kutoka
nchi jirani , kitu ambacho ni kinyume na sheria na hivyo kushikiliwa
katika kitalu namba kumi na moja hadi leo hii. Sasa basi Serikali
haiwezi kuvumilia kuendelea kuwalisha mifugo hao kwa kuwa mnafanya
makusudi na kugoma tutawauza mapato yaingie serikalini endapo muda
niliotoa utaisha bila kufuata agizo la serikali,” aliagiza Kiswaga.
Katika kikao hicho, wafugaji hao walidai hali hiyo haitakoma endapo
serikali haitawapatia maeneo mbadala ya kufugia kutokana na idadi kubwa
ya mifugo waliyonayo ukilinganisha na maeneo waliyotengewa kwa ajili ya
malisho.
Mmoja wa wafugaji hao, Daniel Kwigizile, alisema kuwa wamepokea tamko
hilo la Serikali kwa shingo upande na wanaishauri serikali kutenga
maeneo makubwa zaidi kwa ajili ya malisho la sivyo hali hiyo haitakoma.
Chanzo Gazeti la Habari leo