MAHAKAMA
Kuu kanda ya Bukoba, imetupilia mbali kesi namba moja ya mwaka 2014,
iliyofunguliwa na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani
dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Amani alifungua kesi hiyo, akipinga ripoti ya ukaguzi uliyofanywa na
CAG katika halmashauri hiyo Desemba mwaka jana, kuhusu utekelezwaji wa
miradi ya maendeleo akidai kwamba alionewa.
Ripoti hiyo, iliyosomwa na aliyekuwa CAG, Ludovick Uttouh mbele ya
Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey
Mwanri ilimtia hatiani Amani na aliyekuwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo,
Hamis Kaputa kwamba waliendesha miradi hiyo kwa kukiuka utaratibu wa
kutoshirikisha Baraza la Madiwani na wizara husika.
Katika hukumu yake juzi, Jaji G. J. Mjemmas, alisema kumshtaki CAG ni
jambo linalowezekana lakini kwa suala hilo la kuhusu ripoti ya ukaguzi
haiwezekani CAG kushtakiwa kwasababu alitumwa na Serikali kufanya kazi
yake na imekamilika.
Jaji Mjemmas, aliagiza vyombo vingine vinavyohusika katika suala
hilo, kuchukua hatua za haraka kutekeleza mapendekezo ya ripoti ya CAG
na kusisitiza kwamba kesi hiyo haitaweza kuwepo kabisa huku Amani
akitakiwa kulipa gharama zote za kesi.
Hii si mara ya kwanza kwa Amani kufungua kesi ya kujaribu kupigania
umeya wake, ambao aliupoteza alipotangaza kujiuzulu muda mfupi baada ya
CAG kuwasilisha ripoti yake, lakini baadaye akaibuka na kukana
kujiuzulu.
Kwa sasa, Amani amefungua kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba
dhidi ya Mkurugenzi wa manispaa hiyo, akimtaka amruhusu aingie katika
vikao vya Baraza la Madiwani akiwa mamlaka yake ya umeya na kurejeshewa
haki zake zote za usafiri na mahitaji mengine.
Suala hilo, lilikataliwa na mkurugenzi akisema kuwa hamtambui kwa
sababu kwa mujibu wa maelezo ya barua aliyopewa na serikali ili ampatie
ina maana kwamba yeye si meya tena na hasa kwa kuzingatia tamko lake la
kujiuzulu baada ya CAG kusoma ripoti yake.
Msimamo wa mkurugenzi huyo, ndio ulimlazimu Amani kupitia kwa
mwanasheria wake kufungua shauri katika mahakama hiyo, ambayo juzi
iliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 2 mwaka huu.