BAADHI ya wakulima wa chama cha ushirika cha Kamachumu kilichopo
Wilayani Muleba Mkoani Kagera wamedai kuwa uchaguzi wa kuwachagua
wajumbe wa bodi na mwenyekiti wa chama hicho uliofanyika wiki iliyopita
ulikuwa batili kutokana na sheria namba sita ya ushirika kukiukwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano kabla ya kufanyika
kwa uchaguzi huo mbele ya Afisa ushirika wilayani Missenyi Humphery
Kachelele, aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo walisema sheria hiyo
inakataza mwanachama ambaye ni kiongozi wa siasa kugombea nafasi yoyote
katika ushirika hadi atakapojiuzuru wadhifa wake.
Diocles Rutabana alisema sheria hiyo inakataza wanasiasa kugombea
nafasi za uongozi katika ushirika lakini cha ajabu waliochukuwa fomu ya
kugombea nyadhifa hizo (majina yanahifadhiwa) ni viongozi wa chama cha
siasa kikongwe nchini.
Alisema kutokana na hayo inaonyesha wazi kuwa uchaguzi huo ni batili
kutokana na makao makuu kushindwa kusimamia vyema sheria hiyo na hata
katika suala la ugawaji fomu.
Rutabana alidai kuwa mwenyekiti wao Superi Karugaba aliamua kuficha
fomu hizo ili kumuwezesha kurudi katika nafasi yake pamoja na bodi yake
huku ikiwanyima fursa wanachama waliokuwa na nia ya kuwania nyadhifa
hizo.
“Viongozi wote waliokuwa madarakani walichukuwa fomu pamoja na mtu
mmoja huku kiongozi wa juu wa ushirika akizificha fomu hizo ili wengine
wasipate nafasi ya kugombea,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo wagombea waliochukua fomu walipita bila kupingwa kutokuwa na kukosa upinzani.
Akizungumza katika kikao hicho, Kachelele alisema yeye ndiye
mtafsiriwa sheria hivyo hakuna mtu yeyote anayeweza kumshinikiza katika
hilo.
Hata hivyo aliwauliza wagombea hao iwapo ni wanasiasa ambapo walikana madai hayo na kusema kuwa walishajiuzuru.
Alikwenda mbali zaidi na kutoa onyo kwa wanachama hao ya kuwa iwapo
watasusia uchaguzi huo, atalazimika kuendelea na uchaguzi hata wakibaki
wawili.
Naye mtendaji wa kijiji cha Kamachumu Lenard Anseremy, alisema kuwa
ni mgombea mmoja aliyejiuzulu wadhifa wake lakini waliobaki
walikidanganya kikao hicho kwani hadi sasa bado wanaendelea na shughuli
zao.
Akizungumzia tuhuma za kuficha fomu Karugaba, alisema kuwa madai hayo
hayana ukweli wowote kwa kuwa matangazo yalitolewa ya ugawaji wa fomu
na hakuna wanachama waliofika kuchukua.
Kuhusu kuwania nafasi hiyo kwa miaka 30 pamoja na bodi yake wakiwa ni
walewale, mwenyekiti huyo alisema kuwa suala hilo linapaswa kujibiwa na
msimamizi wa uchaguzi huo
Chanzo:Tanzani Daima
0 comments:
Post a Comment