Home » » RADI YAUA BABA, MAMA NA MTOTO

RADI YAUA BABA, MAMA NA MTOTO

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera,Henry Mwaibambe.
Watu watatu wa familia moja wamefariki dunia papo hapo baada ya kupigwa na radi wakiwa ndani ya nyumba yao katika kijiji cha Byeju Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Henry Mwaibambe, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 24, mwaka huu majira ya usiku kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha.

Kamanda Mwaibambe aliwataja waliokufa katika tukio hilo la kusikitisha kuwa Daud Muonge (35) na mkewe, Fatuma Daud (24) pamoja na mtoto wao, Zaituni Daud, mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Alisema katika tukio hilo, mtu mwingine, Sadam Daud (22), aliyekuwa mgeni wa familia hiyo, alijeruhiwa.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Kagera, limekamata zana haramu za uvuvi ukiwamo mitumbwi inayofanya uvuvi kinyume cha taratibu, injini za boti na watuhumiwa 25 kutokana na msako mkali unaoendelea.

Kamanda Mwaibambe alisema msako uliowawezesha kukamatwa kwa zana hizo ulianza Mei, mwaka huu na unaendelea katika maeneo mbalimbali.

Alitaja zana zilizokamatwa ni injini za boti 10 zinazohofiwa zilipatikana isivyo halali kutokana na namba zake kufutwa, makokoro 38, mbao 1,378,  nyavu saba za kuvulia dagaa, nyavu zenye matundu chini ya sentimita sita 780    na   boti   16   zisizo   na usajili.

Alisema tayari nyavu haramu zilizokamatwa zimeteketezwa kwa moto na watuhumiwa wote waliokamatwa watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya  upelelezi kukamilika.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa